Man City waamua hawatasita

Sergio Aguero (kulia) Haki miliki ya picha AFP
Image caption Licha ya Porto kutangulia kufunga Man City waliibuka na ushindi

Mchezaji wa zamu Sergio Aguero alipata bao dakika za mwishomwisho na kuiwezesha Manchester City, baada ya kufungwa, hatimaye kuweza kujikakamua na kupata ushindi wa magoli 2-1 ilipocheza na Porto ya Ureno, usiku wa Alhamisi, ikiwa ni mechi ya mkondo wa kwanza wa mechi ya ligi ya Europa, kati ya timu 32 ambazo bado zimo katika mashindano.

Porto, ikicheza katika uwanja wa nyumbani, ilikuwa imetangulia kwa kupata bao kupitia Silvestre Varela.

Lakini wageni Man City walipata nafasi ya kusawazisha wakati Alvaro Pereira alijifunga mwenyewe kwa kuuelekeza mpira kwa bega hadi wavuni, kufuatia mkwaju kutoka Yaya Toure, mpira ambao alitazamia utamfikia Balotelli.

Katika mechi ya awali, Ashley Young na Javier Hernandez walifanikiwa kufunga magoli katika kipindi cha pili, na kuishinda Ajax magoli 2-0, na kujiweka katika nafasi nzuri ya kuendelea katika mashindano ya ligi ya Europa.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Manchester United wamo katika hali bora zaidi baada ya kupata mabao ugenini

United walilemewa katika kipindi cha kwanza, na kipa wao David de Gear alifanya kazi ya ziada, na hata kumzuia Siem de Jong kuiandikishia Ajax ya Uholanzi bao.

Lakini wageni Man United walionekana katika hali bora zaidi katika kipindi cha pili, na kuwa na motisha ya matokeo bora hasa Young alipoandikisha bao.

Bao la pili Hernandez bila shaka litaisaidia sana United itakapoikaribisha Ajax katika uwanja wa Old Trafford kwa pambano la mkondo wa pili.

Mechi hiyo itachezwa tarehe 23 mwezi huu wa Februari, na meneja Sir Alex Ferguson ana imani timu yake itajiandikishia nafasi kati ya miongoni mwa timu 16 ambazo zitasalia katika mashindano hayo.

Manchester United inatazamiwa kukutana na Lokomotiv Moscow au Athletic Bilbao.

Licha ya kwamba vilabu mwamba vya Uingereza vimezoea zaidi ligi ya mabingwa na ambao inaheshimika zaidi kushinda Europa, meneja Ferguson ameelezea kwamba wao washatulia baada ya kuondolewa katika michuano ya klabu bingwa, na sasa wanaonyesha ustadi wao kiufundi katika mashindano ya Europa.

Lakini safari ya Stoke kufanya vyema katika mashindano ya Europa inaelekea sio ya heri, baada ya Mehmet Topal kuwapatia wapinzani wao Valencia bado moja katika pambano la mkondo wa kwanza Alhamisi jioni.

Peter Crouch alikaribia kusawazisha, lakini bila shaka kukaribia kufunga sio sawa na kuandikisha bao!