Liverpool yapania kuirarua Arsenal

Mashabiki wa soka jumamosi hii wanasubiri na ubashiri ni mwingi tu kuhusu pambano kwenye uwanja wa Anfield kati ya Liverpool na Arsenal.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Liverpool na Arsenal

Mchuano huu unafanyika wiki moja baada ya Arsenal kuamka kutoka mabao mawili ya Tottenham na kuikandika 5-2 kwenye uwanja wa Emirates.

Ni klabu isiyotabirika, na licha ya masaibu yake Arsenal imesimama katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi, mbele ya Chelsea kwa tofauti ya wingi wa mechi ilizoshinda.

Liverpool itaingia uwanja ikijivunia ushindi wa Kombe la Carling ililoshinda jumapili iliyopita.

Licha ya ushindi huo, hali ya klabu hio katika michuano ya Ligi kuu imekua ikiyumbayumba, ikiwa klabu hio haijaonja ushindi tangu mchuano wake na Wolves mnamo mwezi Januari.

Pande zote mbili zinaingia mchuano kukiwa na mashaka juu ya wachezaji kadhaa wanaoumwa. Nahodha wa Liverpool Steven Gerard anaumwa ikikumbukwa kua aliondolewa wakati wa mechi ya England na Uholanzi.

Arsenal huenda ikamkosa beki wake Tomas Vermerlean ambaye Wenger ametishia kuilalamikia Timu ya Taifa ya Ubelgiji kumtumia mchezaji huyo kwa kipindi kizima cha dakika 90 wakijua kua anasumbuliwa na kisigino.

Pamoja na pambano la jumamosi, Arsenal inajiandalia mechi ya Ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya AC Milan jumanne ijayo.