Liverpool yaloa kwao dhidi ya Arsenal

Bao la ushindi la Robin van Persie katika muda wa nyongeza, limeipatia Arsenal ushindi wa ajabu na kuwaacha nyuma Liverpool kwa tofauti ya pointi 10 katika msimamo wa Ligi Kuu ya England kwenye heka heka za kuwania nafasi nne bora za juu.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Robin van Persie ainyong'onyesha Liverpool

Liverpool walitawala mchezo kwa muda mrefu, lakini Dirk Kuyt alikosa nafasi nzuri ya kufunga kwa mkwaju wa penalti baada ya kuokolewa mara mbili na mlinda mlango wa Arsenal, na vile vile mkwaju wa Luis Suarez nao kukosa kulenga lango na kukonga mlingoti wa lango.

Hatimaye Liverpool walifanikiwa kuongoza wakati mlinzi wa Arsenal Laurent Koscielny alipojifunga mwenyewe alipokuwa katika harakati ya kuokoa mkwaju wa pembeni wa Jordan Henderson.

Lakini Arsenal hawakuzubaa na iliwachukua muda mfupi kipindi cha kwanza kusawazisha kwa bao la Van Persie kwa kichwa na akafanikiwa tena kufunga bao la pili katika dakika za nyongeza kipindi cha pili baada ya kunyanyuliwa mpira wa juu na Alex Song.

Liverpool sasa wanakabiliwa na kibarua kigumu kuweza kumaliza katika nafasi nne za juu, kwani kwa matokeo hayo bado wanaendelea kubakia nafasi ya saba wakiwa na pointi 39, huku Arsenal wakijichimbia katika nafasi ya nne na sasa wamefikisha pointi 49.