Ghana yachelewesha mustakabali wa kocha

Chama cha Kandanda cha Ghana (GFA) kimesema uamuzi juu ya mustakabali wa kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo Goran Stevanovic umecheleweshwa.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Chama soka cha Ghana chachelewesha kumjadili kocha

GFA kilitazamiwa kutangaza siku ya Jumatano iwapo kocha huyo raia wa Serbia ataendelea kuifundisha timu ya taifa au la.

Lakini Chama hicho cha Soka kimeitisha mkutano wa ziada kujadili juu ya uamuzi kuhusiana na kocha huyo.

"Tumeamua kuitisha mkutano wa dharura wa Kamati ya Utendaji kujadili zaidi baadhi ya mambo ambayo yanatakiwa kupatiwa ufumbuzi," alisema Rais wa GFA Kwesi Nyantakyi.

"Tunataka kuwa na uhakika tutakapochukua uamuzi, basi uwe ni uamuzi kwa manufaa ya nchi. Tunahitaji kugusa kila kona," Nyantakyi alieleza hayo kupitia mtandao rasmi wa GFA.

"Tungependa kuwaomba radhi kutokana na ucheleweshwaji huo, lakini imekuwa ni muhimu kufanya hivyo ili tuweze kuchukua uamuzi maridhawa," aliongeza Nyantakyi, ambaye chama chake kimekuwa kikitafuta maoni ya wadau wengi mwezi uliopita.

Kocha huyo amekuwa katika chagizo kubwa tangu kikosi cha Ghana kiliposhindwa kunyakua Kombe la Mataifa ya Afrika 2012 mapema mwaka huu.

Black Stars ya Ghana ilichapwa bao 1-0 na baadae waliokuwa mabingwa Zambia, kabla ya kufungwa na Mali katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu.

Tarehe 22 mwezi wa Februari, wajumbe wa GFA walikutana kutathmini namna timu yao ilivyocheza katika mashindano yaliyofanyika Equatorial Guinea na Gabon - na baadae wakasema watapitia mkataba wa kocha Stevanovic kabla hakijaamua hatua ya kuchukua.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 mkataba wake wa sasa unamalizika mwezi wa Januari mwaka 2013, mwezi ambao michuano ijayo ya Kombe la Mataifa ya Afrika itakapoanza nchini Afrika Kusini.