Imethibitishwa Podolski kutua Arsenal

Klabu ya Arsenal imekubaliana mkataba wa kumsajili mshambuliaji wa Ujerumani Lukas Podolski, mwenye umri wa miaka 26, kutoka klabu ya FC Kolon, kitengo cha michezo cha BBC kimethibitisha.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Podolski kujiunga na Arsenal

Taarifa zilizopatikana zimefahamisha Arsenal italipa kitita cha paundi milioni 10.9 kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji huyo hatari kwa mkataba wa miaka minne kwa mshahara wa paundi 100,000 kwa wiki.

Mlinzi wa Arsenal Per Mertesacker, ambaye anachezea timu ya taifa ya Ujerumani pamoja na mshambuliaji huyo, amesema Podolski amekuwa akimuulizia kuhusu hali ya maisha ilivyo katika uwanja wa Emirates Stadium.

Ameendelea kusema: "Amekuwa akinitumia ujumbe mara kwa mara wa simu ya mkononi, na nimemwambia hapa ni sehemu nzuri ya kufanyia kazi na Arsenal ni klabu nzuri ajabu."

Meneja wa Cologne Stale Solbakken alikiri mwezi uliopita huenda akampoteza Podolski kwa Arsenal.

Klabu mbili kubwa tajiri Lokomotiv Moscow na Anzhi Makhachkala za Urusi, pia zilikuwa zikimuwinda Podolski lakini mshambuliaji huyo alitamka hivi karibuni kwamba pesa sio kitu anachokitazama kwanza.

"Pesa si jambo muhimu sana kwangu, alilieleza gazeti la Ujerumani la michezo la Bild. "Kilicho muhimu kwangu ni kuendeleza kiwango cha mchezo wangu."