Muamba aweza "kutambua" jamaa zake

Fabrice Muamba "ameweza kuwatambua jamaa zake na kujibu maswali kwa usahihi", taarifa iliyotolewa kwa pamoja na klabu yake ya Bolton na hospitali ilieleza.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Afya ya Fabrice Muamba yaimarika

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 ameweza "kupumua bila kutegemea mashine" lakini bado ameendelea kubakia katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa hali ya juu baada ya kuanguka na kuzirai kutokana na matatizo ya moyo siku ya Jumamosi.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na hospitali ya London Chest na Bolton ilisema anaendelea "kuonesha maendelea mazuri ya afya yake".

Taarifa hiyo imeongeza hali yake haikuwa mahututi lakini ameendelea kuwa mgonjwa sana.

Taarifa iliyotolewa mapema ilisema "anaweza pia kuchezesha mikono na miguu yake" lakini "hali yake kwa siku za baadae haitafahamika kwa muda fulani".

Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya England chini ya umri wa miaka 21, amekuwa katika hospitali hiyo ya maradhi ya moyo tangu siku ya Jumamosi wakati wa mechi ya kuwania Kombe la FA hatua ya robo fainali katika uwanja wa White Hart Lane.

Mchumba wake, Shauna Magunda, ambaye ni mama wa mtoto wake mmoja wa kiume aitwae Joshua, alituma ujumbe katika mtandao wa kijamii wa Twitter siku ya Jumatatu jioni akisema: "Sala zenu zote zinafanya kazi nawashuru wote kwa dhati. Kila sala imemfanya aimarike zaidi."

Muamba alizaliwa Zaire, sasa inaitwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na alifika England na umri wa miaka 11 akiwa mkimbizi.

Rais wa Chama cha kabumbu cha DRC Omari Selemani alisema kiungo huyo anaungwa mkono na watu "milioni 65" wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Siku za nyuma mchezaji huyo alikataa jaribio la chama cha kabumbu cha Congo walipomuita aichezee timu ya taifa na badala yake akachagua kuichezea timu ya vijana ya England.