Esperance yabanwa na Brikama ya Gambia

Esperance ya Tunisia imebanwa ilipoanza kampeni ya kutetea ubingwa wao wa Ligi ya vilabu vya Afrika, walipotoka sare ya bao 1-1 dhidi ya klabu ya Gambia ya Brikama United.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Esperance yalazimishwa sare na Brikama

Wajdi Bouazzi aliipatia Esperance bao la kwanza katika mechi ya mzunguko wa pili wa mpambano wa awali mapema tu dakika ya tatu wakati alipotumia makosa ya walinzi.

Bao hilo lilidumu kwa muda wa dakika tisa tu baada ya mshambuliaji wa Brikama Musa Bojang kupachika bao kwa kichwa na kuisawazishia timu yake.

Esperance waliendelea kumiliki mchezo kipindi cha pili lakini walishindwa kupata mwanya wa kufunga.

Washindi wengine wawili wa zamani wa Afrika walikuwa na kibarua kigumu siku ya Jumamosi katika mechi za mzunguko wa kwanza.

TP Mazembe , waliokuwa washindi miaka miwili mfululizo mwaka 2009 na 2010, walibanwa na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.

Kikosi hicho kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kimerejea tena katika mashindano hayo, baada ya kuondolewa mwaka 2011 kwa kumchezesha mchezaji asiyestahiki.

Wakati huo - huo, vigogo wengine wa kandanda wa Tunisia Etoile du Sahel , mabingwa wa mwaka 2007 wa Afrika, walimudu kulazimisha sare ugenini na timu ya APR FC ya Rwanda.

Timu iliyopata ushindi mnono siku ya Jumamosi ilikuwa Al Hilal, timu ya Sudan iliyofika hatua ya nusu fainali mwaka jana, walipoilaza timu ya DFC 9th Arrondissement ya Afrika ya Kati kwa mabao 3-0.

Al Merreikh nao siku ya Jumamosi walibanwa na FC Platinum na kutoka sare ya mabao 2-2 mjini Harare siku ya Jumamosi.