Ahly "haikufurahia" adhabu ya al-Masry

Klabu ya Al Ahly ya Misri imesema "wameshangazwa na kuhuzunishwa" na uamuzi wa kuifungia klabu ya al-Masry kucheza ligi kwa miaka miwili.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ghasia wakati wa mechi ya Port Said, Misri

Vigogo hao wa kandanda wa Cairo wanaamini adhabu hiyo iliyotolewa na Chama cha Kandanda cha Misri siku ya Ijumaa ingekuwa kubwa zaidi ya hiyo.

Mashabiki 74 walikufa mjini Port Said wakati al-Masry ilipoikaribisha Al Ahly tarehe 1 mwezi wa Februari.

"Tumehuzunishwa na kwa kweli tumekasirishwa," mjumbe wa bodi ya Al Ahly Khaled Mortagy aliiambia BBC.

"Tunaamini haki haikutendeka, inapotokea mashabiki 74 wamekufa katika uwanja wa nyumbani wa klabu hii na bado hii ndio adhabu wanayopewa, ni mwaka mmoja tu wanafungiwa kucheza."

"Kwa sababu, kinadharia, msimu huu umemalizika, kwa hiyo wanaposema wanafungiwa miaka miwili, maana yake halisi ni mwaka mmoja tu."

Wakati msimu wa sasa wa ligi ya Misri ukiwa umefutwa tangu kulipotea ghasia za Port Said, al-Masry wataanza kucheza tena soka kwa msimu wa 2013/2014 - ikiwa na maana watakosa msimu wa mwakani tu.

Klabu hiyo ya Port Said pia imefungiwa kuutumia uwanja wake wa nyumbani kwa muda wa miaka mitatu.

Baada ya al-Masry kushinda mabao 3-1 tarehe 1 mwezi wa Februari, mashabiki wake walivamia uwanja na kuwashambulia wachezaji na mashabiki wa Al Ahly.

Wiki iliyopita Mwendesha Mashtaka mkuu wa Misri aliwafungulia mashtaka ya mauaji na uzembe uliosababisha ghasia watu 75.

Mortagy alisema angependa kuona al-Masry ikifungiwa kushiriki Ligi Kuu kwa angalao muda wa miaka mitano, akitolea mfano unaopaswa kufuatwa ilipofungiwa klabu ya Liverpool baada ya mkasa wa Heysel wa mwaka 1985.

Katika tukio hilo, klabu hiyo ya England ilifungiwa kushiriki mashindano ya Ulaya kwa muda wa miaka sita baada ya mashabiki wake kuonesha utovu wa nidhamu uliosababisha vifo vya mashabiki 39, wengi wakiwa wa klabu ya Juventus.

Licha ya Al Ahly kukusudia kukata rufaa kutokana na uamuzi wa Chama cha Kandanda cha Misri, bodi ya klabu hiyo tayari imeshaamua kutocheza mechi yoyote mjini Port Said kwa muda wa miaka mitano ijayo.

Mabingwa hao mara sita wa Afrika, hawakufurahishwa pia na uamuzi wa kuwataka wacheze mechi zao nne katika uwanja usio na watazamaji, baada ya baadhi ya mashabiki wake kufyatua na kurusha miale ya moto, wakati kocha wao Manuel Jose na nahodha Hossam Ghaly pia wamefungiwa mechi nne kwa kuzozana na maafisa.