Arsenal hoi, Chelsea kidedea, City sare

Manchester City walimaliza mchezo kwa mtindo wa aina yake baada ya kuwa nyuma kwa mabao 3-1 kipindi kirefu cha mchezo na kufanikiwa kusawazisha na kuwa mabao 3-3 dhidi ya Sunderland katika uwanja wa Etihad.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Mario Balotelli aliyefunga mabao mawili kwa Man City

Sebastian Larsson alikuwa wa kwanza kuipatia bao Sunderland kabla Mario Balotelli hajasawazisha kwa mkwaju wa penalti kutokana na rafu aliyofanyiwa Dzeko.

Sunderland walijiimarisha kwa kupata bao la pili lililofungwa kwa kichwa na Nicklas Bendtner kabla ya mapumziko na walionekana dhahiri wangeibuka washindi baada ya bao la tatu la Larson.

Lakini Balotelli na Aleksandar Kolarov walibadili hali ya mchezo kwa kusawazsiha, ingawa Manchester City walikuwa wamepoteza rekodi yao ya kushinda uwanja wa nyumbani katika msimu huu.

Licha ya kucheza vizuri na kusawazisha, Man City wanafahamu fika iwapo Manchester United watailaza Blackburn siku ya Jumatatu, mabingwa hao mara 19 watasogea pointi tano nyuma ya City na kuendelea kushikilia usukani.

Lilikuwa pambano la kusisimua hasa dakika za mwisho ambapo Sunderland walionesha kandanda murua na kuweza kuwasumbua kwa muda mrefu wenyeji wao.

Lakini mara tu baada ya kutolewa mlinzi wa kati aliyecheza vizuri sana Matt Kilgallon na nafasi yake kuchukuliwa na Sotirios Krygiakos zikiwa zimesalia dakika 10 mpira kumalizika, wageni walionekana kuparaganyika.

QPR imefanikiwa kupata ushindi muhimu katika jitahada zao za kuepuka kushuka daraja baada ya Samba Diakite kufunga bao lake la kwanza tangu ahamie klabu hiyo na ndio lililoizamisha Arsenal na kupunguza kasi yake ya kushinda.

Adel Taarabt alikuwa wa kwanza kupata bao kwa upande wa QPR baada ya kumpita Thomas Vermaelen na kuachia mkwaju uliojaa wavuni.

Theo Walcott aliisawazishia Arsenal akiwa ndani ya sanduku la QPR na kuachia mkwaju baada ya jitahada zake za awali kugonga mwamba.

Mlinda mlango wa QPR Paddy Kenny alimnyima nafasi ya kufunga Robin van Persie wakati walipobakia wao wawili kabla ya Diakite kupachika bao la ushindi baada ya pasi kutoka kwa Jamie Mackie.

Aston Villa ikiwa nyumbani katika uwanja wao wa Villa Park ilishindwa kuhimili vishindo vya Chelsea baada ya nahodha wao Stiliyan Petrov kugundulika amekumbwa na maradhi ya saratani ya damu.

Mabao yaliyofungwa na Daniel Sturridge na Branislav Ivanovic yaliwasaidia wageni kupata ushindi wa mapema na kumiliki mpira kwa muda mrefu.

Dakika chache baadae zikawa za kuvuti baada ya James Collins kuipatia bao la kwanza Aston Villa, kabla ya Eric Lichaj kusawazisha na kufanya ubao usomeke 2-2.

Lakini sekunde 60 baadae, Ivanovic akafumua mkwaju wa karibu na kupata bao la tatu kabla Fernando Torres kumalizia kazi kwa kufunga bao la nne na la mwisho katika muda wa nyongeza.

Timu ya Everton ikiwa imeimarika ilifanikiwa kuichambua West Brom kwa mabao 2-0, kila bao likipatikana kila kipindi na hivyo kuweza kujinyanyua juu ya mahasuimu wao wakubwa Liverpool katika msimamo wa Ligi Kuu ya England.

Leon Osman alikuwa wa kwanza kuifungia Everton kwa mkwaju wa yadi 20, baada ya kogongeana na Nikica Jelavic, na mpira ukamgonga Gareth McAuley wa West Bromich na kumzubaisha mlinda mlango Ben Foster.

Ni mkwaju wa chinichini wa Victor Anichebe ulizidisha furaha kwa Everton ambao wiki iliyopita waliweza kupata nafasi ya kucheza nusu fainali ya ya Kombe la FA Cup ambao kwa sasa wamejinyanyua hadi nafasi ya saba.

Nafasi nzuri waliyoipata West Brom Albion ilikuwa pale mkwaju wa chini uliopigwa na Paul Scharner ulipopanguliwa na mlinda mlango Tim Howard.

Fulham ilimaliza nuksi ya kupoteza michezo mitatu mfululizo ya ligi baada ya kujipatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Norwich City.

Alikuwa Clint Dempsey aliyeunasa mpira vizuri na kuutumukiza wavuni kabla mlinda mlango wa Norwich John Ruddy kushindwa kuzuia mkwaju wa Bryan Ruiz.

Hadi robo ya kwanza ya mchezo Fulham walikuwa tayari wameshaweka kibindoni mabao mawili.

Fulham mara mbili mikwaju yao iligonga mwamba kutokana na mashuti ya Dempsey na baadae Alex Kacaniklic - lakini mkwaju wa Aaron Wilbraham uliomgonga mchezaji wa Fulham kujaa wavuni na kuipatia Norwich bao la kufutia machozi.

Wigan imeendelea kuwa nafasi ya hatari ya kushuka daraja lakini imefanikiwa kusogea pointi tatu mbele na kuwa sawa na Blackburn nafasi ya 17 baada ya kuilaza Stoke City kwa mabao 2-0 kwenye uwanja wao wa DW Stadium.

Bao la kichwa kipindi cha pili la Antolin Alcaraz liliwapatia Wigan nafasi ya kuongoza.

Ryan Shawcross alipata nafasi nzuri ya kuifungia Stoke kwa kichwa lakini mlinda mlango wa Wigan Ali Al Habsi aliokoa.

Jean Beausejour aliipotezea nafasi nzuri Wigan, kabla Victor Moses kuifungia Wigan bao la pili dakika za mwisho za mchezo.

Matokeo hayo maana yake Wigan imekusanya pointi 28, sawa na QPR pamoja na Blackburn wakiwa juu yao.

Wolves imezidi kudhoofishwa baada ya kuongoza kwa bao moja ikajikuta ikipokea kichapo kutoka kwa Bolton na kujiongezea dhiki mkiani mwa ligi.

Michael Kightly aliipatia bao la kwanza Wolves wakiwa nyuma kwa pointi sita mkiani huku michezo iliyosalia ni sita kabla msimu haujamalizika.

Lakini Martin Petrov akaisawazishia Bolton kwa mkwaju wa penalti baada ya Roger Johnson kumchezea rafu Mark Davies na baadae Marcos Alonso akaipatia Bolton bao la pili na ubao kusomeka mabao 2-1 kwa Bolton.

Kevin Davies aliifungia Bolton bao la tatu kabla Wolves kupata bao la kufutia machozi dakika za mwisho kupitia kwa Matt Jarvis.

Muda unazidi kwenda kwa kikosi cha meneja wa Wolves Terry Connor ambacho hakijashinda katika mechi zake 10 zilizopita.

Connor, bado anahitaji ushindi wake wa kwanza tangu alipochukua hatamu za umeneja. Wolves waliongoza kipindi cha kwanza lakini iliwawia shida kutumbukiza mpira wavuni.