Tunaweza kuibwaga Barcelona

Di Matteo Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kocha wa Chelsea Di Matteo anaamini wanaweza kuzuka na mbinu za kuishinda Barcelona

Anayeshikilia cheo cha meneja wa Chelsea wa muda, kocha Roberto di Matteo, anasisitiza kwamba wao wanaweza kuzuka na mbinu ambazo zitawasaidia katika kibarua kigumu cha kuiangusha Barcelona katika mechi za nusu fainali za klabu bingwa barani Ulaya.

Barcelona ndio kizuizi kati ya Chelsea na fainali ya mjini Munich, nchini Ujerumani, mwezi Mei.

Timu ya The Blues (jina la utani la Chelsea) ilimaliza hatua ya robo fainali kwa kuishinda Benfica ya Ureno kwa jumla ya magoli 3-1, na ikipata ushindi wa magoli 2-1 katika mechi ya uwanja wa nyumbani wa Stamford Bridge usiku wa Jumatano.

Di Matteo anasisitiza kwamba Chelsea hawana wasiwasi kutokana na historia, wakati Barcelona, ambao wengi wanasema huenda wakaibuka washindi msimu huu, walipoishinda Chelsea katika nusu fainali ya mwaka 2009, wakati Andres Iniesta alipowafungia bao Barcelona mara tu baada ya muda wa kawaida wa mechi kumalizika, na kuwawezesha wageni kufuzu.

"Itakuwa ni jambo la kusisimua sana kucheza mechi mbili na kati ya vilabu bora zaidi duniani. Tutapata mbinu ambayo itawafaa wachezaji wetu kuweza kupambana na Barcelona", alielezea Di Matteo.

"Itakuwa ni mchanganyiko wa kucheza kwa kadri ya uwezo wetu na vile vile kutambua uwezo wao", alifafanua.

Klabu ya Chelsea ilihisi bahati haikuwa yake ilipoondolewa na timu ya meneja Pep Guardiola mwaka 2009, na walilalamika vikali kuhusiana na namna mwamuzi kutoka Norway, Tom Ovrebo aliyosimamia mechi hiyo.