Ushindi ni wa mashabiki wa Liverpool

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Wachezaji wa Liverpool wakishangilia ushindi

Golikipa wa Liverpool Brad Jones amesema ushindi wa magoli 3-2 wa Liverpool dhidi ya Blackburn ni kutokana na kuungwa mkono na mashabiki tangu kifo cha mwanae wa kiume.

Mlinda mlango huyo nambari tatu katika kikosi cha Liverpool aliokoa penalti moja na kufungwa penalti nyingine, katika mechi yake ya kwanza ya ligi kuu ya England.

" Imekuwa miezi 18 migumu na matokeo yake natoa shukrani zangu kwa mashabiki kwa kuniunga mkono," alisema Jones mwenye umri wa miaka 30, ambaye mtoto wake mwenye umri wa miaka mitano, Luca, alifariki dunia kutokana na saratani ya damu mwezi Novemba.

Jones aliongeza kuwa mpenzi wake mwanamitindo Dani Lawrence, alijifungua mtoto wa kiume hivi karibuni,jina lake ni Nico.

"Na kwa kuzaliwa mtoto wangu, Nico, siku ya Jumatano, hii imekuwa wiki nzuri sana," alisema mchezaji huyo raia wa Australia.

Jones aliingia kama mchezaji wa akiba mnamo dakika 26 katika mechi yao na Blackburn kwenye uwanja wa Ewood Park baada ya golikipa nambari mbili Alexander Doni - kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya mchezaji Junior Hoilett.

Jones aliokoa penalti iliopigwa na Yakubu, lakini mchezaji huyo wa zamani wa Middlesbrough alifungwa penalti ya pili na mshambuliaji huyo wa Rovers katika kipindi cha pili baada ya kumsukuma Yakubu.