F1 itafanyika Bahrain

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption mashindano ya langalanga

Shirikisho la mbio za magari ya Formula 1 limethibitisha kuwa mashindano ya Bahrain Grand Prix yatafanyika tarehe 22 Aprili

Uamuzi huo umekuja baada ya wasiwasi kuhusu matukio katika nchi hiyo ya Ghuba, ambapo kumekuwa na hali tete tangu kutokea kwa maandamano mwezi Februari mwaka 2011.

Shirikisho la FIA limepata shinikizo la kufutilia mbali mashindano hayo huku kukiwa na wasiwasi kuhusu usalama.

Lakini taarifa kutoka kwa FIA inasema "imeridhishwa na hatua za usalama zilizochukuliwa tayari kwa mashindano hayo ya Formula 1".

Waandamanaji nchini Bahrain wametaka mashindano hayo yasifanyike. Familia ya kifalme ambayo inatawala nchi hiyo, imetakiwa kuimarisha haki za binadamu na kufanya mabadiliko,shinikizo hizo zimetoka kwa wafuasi wa madhehebu ya Shia walio wengi, na wanawashtumu wafuasi wa madhehebu ya Sunni walio wachache kwa kufanya ubaguzi.

Shinikizo zimezidi katika wiki kadha zilizopita kutokana na maandamano kuendelea katika maeneo ya makazi ya watu wa madhehebu ya Shia.