Kipsang na Keitany

Wilson Kipsang
Image caption Kipsang alikaribia kuvunja rekodi ya mashindano ya London Marathon

Wilson Kipsang na Mary Keitany kutoka Kenya walichukua ushindi kwa kishindo katika mashindano ya Jumapili ya mbio za London Marathon mwaka 2012.

Katika mbio za wanaume, Kipsang aliweza kuongoza katika maili saba za mwisho, na ilikuwa nusra avunje rekodi ya mashindano ya London.

Alimaliza kwa muda usiokuwa rasmi wa saa 2:04.44.

Mkenya mwenzake Martin Lel alifanikiwa kumpita mwanariadha wa Ethiopia, Tsegaye Kebede, na ambaye ameshawahi kuwa mshindi wa mashindano ya London, na kumaliza katika nafasi ya pili, katika kasi ya juu mno katika kumalizia mashindano.

Image caption Keitani amefanikiwa kuutetea ubingwa wake wa London Marathon

Kebede, aliyemaliza wa tatu, alifanikiwa kuwazuia Wakenya kuzoa nafasi zote tatu za mwanzo kwa upande wa mbio za wanaume, lakini kwa upande wa kina dada juhudi za Waethiopia hazikufanikiwa.

Mary Keitany alifanikiwa kuhifadhi ubingwa wake kwa mwaka wa pili mfululizo, kwa kushinda katika muda wa 2:18.37.

Muingereza wa kike aliyefanya vizuri zaidi ni Claire Hallissey, na alifanikiwa kufuzu kuingia mashindano ya Olimpiki.

Paula Radcliffe na Mara Yamauchi tayari walikuwa wamefuzu.