Liverpool 0 Fulham 1

Fulham Haki miliki ya picha Getty
Image caption Timu ya Fulham kwa mara ya kwanza ilipata ushindi katika uwanja wa Liverpool wa Anfield

Bao la kujifunga mwenyewe la Martin Skrtel lilileta masikitiko mengi usiku wa Jumanne wakati walipoikaribisha Fulham katika uwanja wa Anfield, na kuwasaidia wageni kuandikisha historia, ikiwa ni mara yao ya kwanza kupata ushindi katika uwanja huo.

Lakini inaelekea meneja wa Liverpool, Kenny Dalglish, hakuwa na wasiwasi mno, kwani tangu mwanzo aliichezesha timu dhaifu, wachezaji wake mahiri akiwapumzisha na anakusudia kuwatumia kikamilifu katika pambano la fainali la Kombe la FA mwishoni mwa wiki.

Liverpool walipata nafasi za kusawazisha, lakini Mark Schwarzer hakuwa mbunifu katika kumalizia na kuelekeza mikwaju vyema.

Fulham pia walishindwa kujiongezea mabao, kwani Kerim Frei aligonga mwamba, na kipa wa Liverpool Doni pia aliweza kuiokoa timu yake kutoka kwa makombora zaidi ya Pavel Pogrebnyak na Clint Demsey.

Matokeo hayo yanamaanisha Fulham sasa ina pointi 49, sawa na Liverpool.

Liverpool imo katika nafasi ya nane, na msimu huu imeshinda mechi tano tu, kati ya 18, na sasa wameachwa nyuma kwa pointi tatu na Everton, ambao pia usiku wa Jumanne walikamilisha mechi yao kwa sare ya 1-1 dhidi ya Stoke City.

Bila shaka mechi hii itakumbukwa na mashabiki wengi wa Liverpool, na ambao watajiuliza timu yao imejiandaa vipi katika kupambana na Chelsea katika fainali ya Kombe la FA, Jumamosi, tarehe 5 Mei.