Lewis Hamilton aadhibiwa

Lewis Hamilton Haki miliki ya picha AFP
Image caption Aadhibiwa katika mashindano ya Uhispania

Dereva wa timu ya McLaren, Lewis Hamilton, sasa amewekwa kando na hataweza kuwa miongoni mwa madereva ambao wataweza kupata pointi katika mashindano ya Jumapili ya langalanga ya Formula One nchini Uhispania, baada ya kuliacha gari lake hatua chache kabla kituo cha mwisho cha kumalizia mashindano.

Hamilton alifuzu kuwa wa kwanza kuanza mashindano Jumapili, lakini sasa amepangwa katika nafasi ya mwisho.

Aliarifiwa asimame, kwani gari lake lilikuwa halina mafuta ya kutosha alipokaribia kituo cha mwisho, kwani kulingana na sheria za mashindano hayo, ni lazima uwe na angalau lita moja ya mafuta, ili yaweze kukaguliwa.

Maafisa wa mashindano hayo walikataa hatua ya McLaren ya kujitetea, kwamba ukosefu wa mafuta ni hali ambayo ilimsaidia Hamilton kujiweka katika nafasi bora zaidi ya mashindano hayo.

Kulingana na kifungo cha sheria kuhusiana na mafuta, kipengele 6.6.2 juu ya kanuni za kiufundi, kinaeleza kwamba "washindani wote lazima kuhakikisha kwamba angalau wana kiasi cha lita moja ya mafuta, ambayo yanaweza kutolewa wakati wowote wakati wa mashindano ili kufanyiwa ukaguzi".

Sheria hizo pia zinaeleza kwamba "ikiwa kipimo hicho cha mafuta kitahitajika baada ya kipindi cha mashindano ya mazoezi, gari linalohusika lazima kuendeshwa kwa nguvu zake zenyewe hadi kituo", yaani pasipo kusukumwa au kuvutwa.

Sheria za Formula One zinasisitiza kwamba gari lazima kurudi katika kituo likiwa na angalau lita moja ya mafuta, kwani kuwa na chini ya kipimo hicho humnufaisha dereva na kujiweka katika hali bora zaidi ya ushindani akijilinganisha na madereva wenzake.

Ingawa hali hiyo haikumsaidia Hamilton katika kuongoza katika mashindano ya mazoezi alipomtangulia Pastor Maldonado wa timu ya Williams kwa muda wa sekunde 0.578, wasimamizi wa mashindano walihisi hawanabudi kuiadhibu timu ya McLaren.

Taarifa ya maafisa hao ilieleza: "Kuna mtu katika timu aliyeweka mafuta yasiyotosha katika gari, na ikabidi hatua ya kulisimamisha gari hilo kabla ya kufikia kituo ili kupata kipimo fulani cha mafuta kwa madhumuni ya kuyakagua".

Kwa upande wake, taarifa ya McLaren ilielezea: "Tunakiri maafisa wa mashindano hawakukubaliana nasi jinsi tulivyojitetea kwamba kuhusiana na hali hii, haikutoa nafasi dereva kuweza kujinyakulia pointi zaidi".

Martin Whitmarsh, mkuu wa timu ya McLaren, alikuwa amejitetea kwa kuelezea kwamba kutokana na tofauti kubwa ya muda kati ya Hamilton na dereva Maldonado kutoka Venezuela, Hamilton ilifaa aachiwe kuanza katika nafasi ya kwanza Jumapili.

"Kulikuwa na tofauti kubwa, na kulingana na hali ilivyo hivi sasa katika Formula One, hamna shaka angeliruhusiwa kuwa mwanzo", alilalamika Whitmarsh.

Lakini hayo yalikataliwa, na Maldonado, kwa mara ya kwanza katika maisha yake, ataanza wa kwanza katika mashindano Jumapili, na Fernando Alonzo naye wa timu ya Ferrari akisogezwa mbele hadi nafasi ya pili.

Bila shaka Hamilton atajiuliza ni kwa nini anakabiliana na tatizo hilo kwa mara ya pili.

Kanuni kuhusiana na mafuta zilibadilishwa na bodi ya dunia ya mchezo wa mashindano haya, FIA, wakati tatizo kama hilo lilipompata Hamilton mwaka 2010 katika mashindano ya Canada ya Grand Prix.