Chelsea kazi nzito Ujerumani

Chelsea
Image caption Wachezaji wa Chelsea wana kibarua kigumu

Hatimaye Chelsea wanaingia uwanjani Jumamosi katika hatua ya mwisho ya jitihada zao za kutwaa Kombe la Mabingwa Ulaya.

Chini ya kocha wa muda, Roberto Di Matteo, Chelsea wana kazi ngumu bado, kwani watakuwa Allianz Arena, nyumbani kwa Bayern Munich, wakikabiliana nao kwenye fainali.

Kama ndoto vile, katika nusu fainali, Chelsea iliwashangaza wengi, kwa kuisambaratisha timu bora Ulaya na duniani, Barcelona.

Fainali ya wikendi hii ni wazi itakuwa ngumu kwa timu zote, huku Chelsea wakiwa wameshajijenga kisaikolojia na kujiamini kwamba wanaweza.

Hata kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes anaamini kwamba, kwa timu yake kucheza nyumbani, ina nafasi kidogo tu juu ya Chelsea, anaosema ni hatari.

Ni mchezo unaosubiriwa na wengi, utakaokusanya mashabiki wengi katika uwanja wenye uwezo wa kubeba watu 66,000 katika mechi za kimataifa.

Hofu

Chelsea wanaingia uwanjani wakijua ugumu wa mechi yenyewe, licha ya ukweli wa kuifunga Barcelona, kwa sababu Bayern Munich ni timu ngumu popote inapochezea, lakini pia itakuwa ikishangiliwa na maelfu ya mashabiki wake.

Bila shaka kocha Di Matteo atatathmini na kutumia kila mwanya, iwe wa kisoka au kisaikolojia kwa ajili ya kuwaweka wachezaji wake kwenye nafasi nzuri.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Bayern Munich watakuwa nyumbani

Wanatakiwa kuondoa hofu na kuweka kando uzito wa mazingira ya mchezo huo wa ugenini ili kutwaa zawadi kubwa zaidi ya soka katika bara la Ulaya.

Si rahisi hata hivyo, kwa Chelsea kurudia mbinu walizotumia Liverpool walipojikuta katika mazingira ya aina hii mwaka 1984 walipokabiliana na AS Roma kwenye uwanja wa Stadio Olimpico.

Katika mechi hiyo iliyofanyika Roma, Italia nyumbani kwa AS Roma, Liverpool waliwabana wenyeji wao na kutoka sare ya bao 1-1 na baadaye kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 walipopigiana mikwaju ya penalti.

Liverpool katika mechi hiyo hawakubabaishwa na mashabiki wa AS Roma, wakaenda sambamba na nyimbo walizokuwa wakiimba na kuzichukulia kana kwamba ni za dimbani kwao Anfield.

Taratibu wakawachota na kuwanyamazisha wapinzani wao nyumbani kwao.

Mark Lawrenson wa Idara ya Michezo ya BBC alicheza kwenye fainali hiyo na bado anakumbuka mambo yalivyokuwa hata leo.

“Kwenye chumba cha kubadilishia nguo tulicheka sana tukiwa na baadhi ya watu mashuhuri (kama Kenny Dalglish na Ian Rush).

“Tulishazunguka uwanjani kukabiliana na kuzoea mazingira yasiyokuwa mazuri kwetu. Hilo lilikuwa wazo la Graeme Souness (mchezaji wa Liverpool enzi hizo),” anakumbukia Lawrenson.

Ugenini

Anasema kwamba kabla ya mchezo pia walipata fursa ya kuimba, kuonyesha jinsi walivyojiamini, kocha wa AS Roma, Nils Liedholm aliyekuwa akikamilisha kuwapanga wachezaji akapigwa butwaa, huku wachezaji wake wakionekana kutoamini.

Lawrenson anasema ikiwa Chelsea wanaweza kupata kitu cha aina hiyo kitakachowapa moyo na kuinua morali, ni muhimu kufuata nyayo zao, kwa sababu hatimaye Liverpool walifanikiwa.

“Wasikubali Bayern wawape mashabiki wao kitu cha kushangilia mapema hata kidogo. Mchezo unatakiwa uwe umetulia kama maji ya mtungi, ikiwa hivyo, natabiri mambo yatakuwa mazuri kwa Di Matteo,” anasema.

Alan Hansen, mchezaji mwingine aliyekuwa akicheza nafasi ya ulinzi Liverpool sambamba na Lawrenson, naye anakumbuka jinsi walivyoibuka na kuanza kuimba wakijipa moyo ugenini.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Roberto Di Matteo ameshangaza wengi

“Lazima walituangalia (AS Roma) na kudhani tumeingiwa wazimu, lakini ukweli ni kwamba kilikuwa kiashirio cha umoja na ushirikiano tuliokuwa nao. “Tulishikamana kabisa, na hicho ndicho Chelsea wanachotakiwa kufanya wanapocheza fainali ya Ligi ya Mabingwa nyumbani kwa wapinzani wao. Wawe ndio maneno ya mwisho kwa kila mmoja – washikamane maana bila hivyo mnakuwa si chochote kwenye michezo hii.

“Yaweza ikaonekana kana kwamba mazingira si ya haki kwa Chelsea, lakini Chelsea siku zote walikuwa wanajua ni wapi fainali ingeenda kuchezwa.

“Unaweza pia kufikiria kwamba kwa kucheza kwenye uwanja wao wa nyumbani, shinikizo litaongezeka kwa Bayern, lakini ngoja niseme, shinikizo zinakuwapo kila mahali,” anaeleza mkongwe huyo wa soka.

Kadi nyekundu

Ukiachilia mbali suala la kucheza nyumbani au ugenini enzi hizo, AS Roma ilipewa nafasi kubwa ya kushinda kwa sababu ilikuwa imeahidiwa kitita kikubwa mara 10 ya Liverpool.

Liverpool walipata £6,000 wakati AS Roma walikuwa wapate zawadi ya £64,000

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Terry akioneshwa kadi nyekundu

Pengine mtu mpweke zaidi duniani usiku huo atakuwa John Terry. Huyu tamaa yake kubwa ilikuwa kutumia maarifa yote ili washinde, lakini hataruhusiwa kucheza kutokana na kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo dhidi ya Barcelona.

Hata hivyo, ikumbukwe kwamba katika mechi ya nusu fainali ya pili dhidi ya Barcelona, Chelsea walicheza muda mrefu zaidi bila Terry, tena wakiwa 10 dhidi ya 11 wa adui zao na bado wakavuka.

Zaidi ya hapo ni kwamba Chelsea itakuwa na wachezaji wake mahiri kama Frank Lampard, Ashley Cole, Didier Drogba na kipa aliyefanya kazi ya ziada kwenye mechi zote zilizopita, Petr Cech.

Wengine ambao wamezuiwa kucheza kwa upande wa Chelsea ni Branislav Ivanović, Raul Meireles na Ramires.

Habari njema pia za kuwapo wachezaji Gary Cahil na David Luiz zinawaweka wachezaji wenzao, kocha na mashabiki kujawa imani zaidi kwamba wataweza kufanya vizuri.

Hata hivyo, Bayern Munich ni timu ya kuangalia vizuri, kwa sababu ni kikosi kilichojipanga na kinachocheza kwa nguvu na akili.

Wachezaji wake wanaweza kuwatia wehu Chelsea kwa kuwatembeza uwanja mzima, wakiwavuta huku na kule, hata kama Chelsea wangependa kutumia mtindo wa kulinda zaidi lango lao.

Wakongwe

Walifanikiwa kufanya hivyo baada ya kupata bao la kwanza la kushitukiza lililowaacha wengi midomo wazi katika nusu fainali ya kwanza dhidi ya Barcelona.

Chelsea walirudia aina hiyo ya mchezo kwenye Uwanja wa Camp Nou jijini Madrid, Hispania, huku wakifanya mashambulizi ya kushitukiza, kama yaliyowapatia mabao kupitia kwa Ramires Santos do Nascimento na la pili dakika za lala salama kupitia kwa mkongwe aliyesahaulika, Fernando Torres.

Katika hili, Chelsea wanatakiwa kuwa makini na Bayern Munich, kwa sababu inao wakongwe wanaoweza kuwa tishio kubwa kwa klabu hiyo ya London na kuwafanya waondoke Munich kwa aibu usiku huo.

Hao ni pamoja na Franck Ribery na Arjen Robben wenye uwezo mkubwa wanapokuwa dimbani, wakisaidiwa na wachezaji wa nyuma ambao wamekuwa wakihakikisha kipa wao hasulubiwi.

Imefanikiwa

Yote kwa yote, kocha Di Matteo atakuwa ameshasoma na kupanga mbinu za kukabiliana nao, huku wachezaji wakisema kama waliwaweza Barcelona, kipi kitashindikana kwa Bayern?

Labda hilo ndilo linaloangaliwa pia na kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes, ambaye atakuwa uso kwa uso na Di Matteo, kila mmoja akiwapanga wachezaji wake ili hatimaye acheke wa mwisho.

Kama ni uzoefu, pengine ni vigumu kupata kocha wa kumfananisha na Heynckes.

Huyu alianza ukocha wakati Di Matteo hajaanza hata kucheza mpira wa kulipwa. Ni huyu aliyeiwezesha Real Madrid kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1998.

Licha ya uzoefu na mafanikio yake mengi, kocha huyo mwenye umri wa miaka 67 anasema anaihusudu Chelsea inavyojituma tangu Di Matteo alipoteuliwa kuwa kocha wa muda Machi mwaka huu.

Haoni sababu ya kubweteka, kwa vile anaamini Chelsea imekuwa ikibadilika kuendana na matakwa ya mazingira kwa kila mechi, na kwa hilo imefanikiwa mara kadhaa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Chelsea wakishangilia ushindi dhidi ya Barcelona

“Unaona Chelsea wanaweza kucheza mifumo tofauti. Walicheza tofauti kabisa walipokabiliana na Benfica (ya Ureno, kwenye robo fainali) ikilinganishwa na walivyocheza dhidi ya Barcelona.

“Natarajia kwamba Chelsea itakuwa tofauti kidogo (itakapocheza na Bayern Munich) na ilivyokuwa ikicheza na Barcelona. Kwa hakika timu hii imekuwa ikipita kwenye kipindi kizuri katika wiki zilizopita.

Wanacheza soka nzuri zaidi na yenye mafanikio," Anasema Heynckes anayetafuta rekodi ya kuwa kocha wa nne kupata kombe hilo akiwa na timu tofauti.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi aliyechukua hatamu za Bayern Munich kwa mara ya tatu kipindi kilichopita cha majira ya joto, anawaheshimu wachezaji wa Chelsea.

“Wana wachezaji uzeofu mkubwa katika timu yao na ni wazi kwamba maveterani hao, wachezaji walioichezea Chelsea kwa muda mrefu wanataka kusinda kitu fulani kikubwa. Hiyo ni hatari kubwa kwetu.

“Mchezo utakuwa wazi na nafasi za timu kushinda ni nusu kwa nusu, lakini huenda tukafaidika kidogo kwa kucheza hapa nyumbani,” anasema kwa matumaini mtaalamu huyo wa soka.

Pamoja na kufaidika kwa kuchezea nyumbani, Heynckes anajua kwamba mechi hii muhimu inatoa fursa kwake kuandika historia kwa timu aliyoipa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mara mbili mfululizo – 1988/89 na 1989/90.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Wengi walitarajia Barcelona kucheza fainali

“Ni jambo la kipekee kucheza fainali kwenye uwanja wenu, ni kitu kisichokuwa cha kawaida, kwa hiyo ushindi kwetu litakuwa jambo kubwa sana,” anasema.

Hata hivyo, kitu kinachomuumiza kichwa mkongwe huyo aliyepata kuwa VfL Borussia Mönchengladbach ni jinsi ya kuziba pengo la nyota wake watatu ambao hawatacheza Jumamosi hii.

Kocha mpya

Hao ni Holger Badstuber, David Alaba na Luiz Gustavo. Kocha huyo anasema angefurahi zaidi ikiwa wachezaji wote muhimu kwa timu hizo mbili wangekuwa dimbani, ili wachuane ipasavyo.

Hivi sasa Kombe la Ubingwa wa Ulaya halina mwenyewe, baada ya Barcelona kulitema walipotandikwa na Chelsea kwa uwiano wa mabao 3-2.

Barcelona walitwaa kombe hilo Mei 28, 2011 katika Uwanja wa Wembley, Uingereza, baada ya kuwafunga Manchester United kwa mabao 3-1.

Barcelona walitawala mchezo huo kwa kiasi kikubwa, na mabao yao yalifungwa na Pedro Rodríguez, Lionel Messi na David Villa.

Wayne Rooney ndiye alifunga bao la United na kuzifanya timu kwenda mapumziko zikiwa sare ya mabao 1-1.

Jumamosi hii, wadau wa Chelsea wana hamu ya kuiona timu yao ikitwaa kombe hilo na kujiwekea heshima kote barani Ulaya.

Licha ya kombe na zawadi, Di Matteo anaangaliwa kwa karibu, kwa sababu uamuzi wa nani awe kocha mpya utatolewa baada ya fainali hizi.

Wakongwe

Chelsea haikumaliza ligi mahali pa kuweza kujidai wala kufuzu uwakilishi wa Ulaya, kwani iliishia nafasi ya sita, ikijifariji kwa kutwaa Kombe la FA na kufika fainali hii muhimu.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chelsea, Ron Gourlay alisisitiza wiki moja kabla ya mechi hii kwamba hatimaye ya Di Matteo haingeamuliwa kabla ya mashindano hayo makubwa zaidi barani Ulaya kumalizika.

Pengine Di Matteo hajafanya vya kutosha kiasi cha kukabidhiwa mikoba ya klabu hiyo kongwe moja kwa moja, na uamuzi wa mwisho waweza kutoka kwa mmiliki wa klabu, bilionea wa Kirusi, Roman Abramovic.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Chelsea wameshinda Kombe la FA

Huenda fainali hii ikawa nafasi ya mwisho kwa baadhi ya wachezaji wakongwe wa klabu hiyo kama Didier Drogba kuichezea, japokuwa Gourlay anasema mazungumzo kuhusu mkataba wake unaomalizika majira haya ya joto yanaendelea.

Licha ya kunyakua Kombe la FA kwa kuwafunga Liverpool, Chelsea ilikuja kufungwa na wababe hao wa Anfield wiki iliyofuata kwa mabao 4-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England (EPL) na kutia uchachu kwenye tamu ya ushindi wao wa awali.

Mtaliano Di Matteo alipewa nafasi ya muda ya ukocha baada ya kufukuzwa kwa kocha kutoka Ureno,

Andre Villas-Boas, maarufu kama AVB, ambaye matokeo ya mfululizo katika siku zake za mwisho hayakuwa yakiridhisha.

Alipoondolewa, wakuu wa Chelsea walisema walidhani hatua hiyo ilikuwa muhimu, kwa sababu walitaka kumaliza EPL kwenye nafasi nzuri.

Lakini pia walikuwa wakizingatia ushiriki wao kwenye michuano ya Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Usikiose kuungana naye Salim Kikeke na Wazir Khamsin kwa matangazo ya moja kwa moja ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC pamoja na redio washirika, katika matangazo maalum ya Ulimwengu wa Soka kuanzia saa tatu usiku za Afrika Mashariki, kufahamu ni klabu kipi kitaibuka bingwa barani Ulaya.