Nadal amshinda Djokovic

Rafael Nadal Haki miliki ya picha Getty
Image caption Nadal sasa anashikilia nafasi ya pili kwa ubora wa mchezo miongoni mwa wachezaji wa kiume duniani

Rafael Nadal, mchezaji wa Uhispania, alifanikiwa kumshinda mchezaji bora zaidi duniani wa kiume, Novak Djokovic katika mashindano ya Italia Open, na kupata ubingwa wake wa sita katika mashindano hayo ya Italia.

Nadal alipata ushindi wa 7-5 6-3 katika fainali hiyo ambayo ilichezwa Jumatatu baada ya kuahirishwa siku ya Jumapili kutokana na mvua kunyesha mno mjini Roma.

Ushindi huo umemweka Nadal katika nafasi ya pili katika orodha ya wachezaji bora zaidi katika mashindano ya wanaume duniani.

Kabla ya mashindano ya Jumatatu, Djokovic, raia wa Serbia, amekuwa akimshinda Nadal mfululizo katika mashindano saba yaliyopita, kabla ya kuanza kuibuka tena kama mshindi katika fainali ya Monte Carlo Masters mwezi uliopita.

Sasa Nadal amemshinda katika fainali mbili za mwisho walizokutana.

Nadal alisema: "Mawazo ya ushindi yalinijia wakati muwafaka, kwani kumshinda Novak, unahitaji kuwa katika hali yako bora zaidi ya uchezaji, kwani yeye hukusukuma hadi mjwisho katika pambano lote.

"Nadhani kiakili nilikuwa katika hali thabiti kila wakati muhimu nilipohitajika kuwa hivyo."