Mikwaju ya penalti haifai

Penalti Haki miliki ya picha Getty
Image caption Blatter amependekeza juhudi zifanywe kutafuta mbinu ya kukamilisha mechi iliyokwisha kwa sare baada ya dakika 120

Rais wa shirikisho la kimataifa la soka, FIFA, Sepp Blatter, amemtaka Franz Beckenbauer, ambaye anashikilia madaraka ya rais wa Bayern Munich kama wadhifa wa kumheshimu, kufikiria juu ya mbinu mpya za kukamilisha mechi iliyokwisha sare, badala ya "msiba" kupitia mikwaju ya penalti.

Beckenbauer ni mkuu wa kikundi kilichoteuliwa na FIFA na kukabidhiwa jukumu la mapendekezo ya kubadilisha au kutunga sheria ambazo zitatumika katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014.

"Soka inaweza kugeuka ikawa ni msiba ikiwa itaingia katika mikwaju ya penalti", ameelezea Blatter.

"Kandanda haifai kuwa mchezo wa mmoja kwa mmoja. Kandanda inapoingia katika mikwaju ya penalti, basi inapoteza kivutio".

Aliongezea: "Pengine Franz Beckenbauer na kundi lake la mapendekezo ya 2014 anaweza kutueleza suluhu, pengine sio sasa, lakini siku zijazo."

Ushindi wa fainali ya ligi ya klabu bingwa barani Ulaya msimu huu iliamuliwa kwa mikwaju ya penalti, wakati Chelsea walipopata ushindi, ilhali ni Bayern Munich waliovuma katika mechi nzima.

Hii ilikuwa ni mara ya kumi kwa fainali ya Ulaya kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti.

Kabla ya mikwaju ya penalti kuanza kutumika katika miaka ya sabini, mechi sare ziliamuliwa kwa kuchezwa upya, na nyingi zilikwisha kwa sare tena.

Baadhi ya mechi pia ziliamuliwa kwa kurusha sarafu juu, mfano ikiwa ni nusu-fainali ya Ulaya mwaka 1968, wakati Italia ilipoishinda Sovieti baada ya kurushwa sarafu.

Zambia pia ilishinda Kombe la Mataifa ya Afrika kupitia mikwaju ya penalti mwaka huu, kwa kuishinda Ivory Coast.

Mara mbili Kombe la Dunia pia limeamuliwa kwa penalti, wakati Brazil ilipoishinda Italia mwaka 1994, na Italia ikaishinda Ufaransa katika mashindano ya 2006.