Schumacher kasi zaidi Monaco

Dereva wa timu ya Mercedes, Mjerumani Michael Schumacher, alionyesha maarifa ya miaka mingi katika mashindano ya Monaco ya Grand Prix, na kuandikisha muda wa kasi zaidi.

Image caption Mambo yamekuwa yakimwendea mrama tangu kurudi katika mashindano baada ya kustaafu

Lakini baada ya kuadhibiwa, dereva huyo sasa ataanza katika nafasi ya sita, na dereva wa Red Bull, Mark Webber, sasa akipangwa kuwatangulia madereva wote katika mashindano ya Jumapili.

Webber alikuwa ameshindwa na Schumacher kwa muda wa sekunde 0.08.

Mwenzake Schumacher katika timu ya Mercedes, Nico Rosberg, alimaliza katika nafasi ya tatu katika mashindano hayo ya Jumamosi ya mazoezi.

Dereva wa Uingereza, Lewis Hamilton wa timu ya McLaren alikuwa wa nne, huku Romain Grosjean wa timu ya Lotus akiwa katika nafasi ya tano.

Jenson Button, aliyeshikilia nafasi ya 13, ataanza katika nafasi ya 12, baada ya Pastor Maldonado pia kuadhibiwa.

Baada ya kuandikisha muda wa kasi zaidi, Schumacher alisema: “Hayo yanathibitisha kile ambacho nimekuwa nikiamini kwa muda mrefu, kwamba huwa kuna wakati maalum wa kufanya juhudi zako zote ili kupata ufanisi.”

Mkuu wa timu ya Mercedes, Ross Brawn alisema: "Lazima nikiri kwamba machozi yalitaka kunidondoka. Mambo yamekuwa magumu kwake tangu kurudi katika mashindano haya, lakini mwishoni mwa wiki hii amekuwa katika hali nzuri mno."