Mark Webber aibuka mshindi Monaco

Mark Webber aliibuka mshindi katika mashindano ya langalanga ya Monaco GP siku ya Jumapili, huu ukiwa ni ushindi wake wa pili huko katika kipindi chini ya miaka mitatu, na akiwatangulia madereva Nico Rosberg kutoka Ujerumani, na wa timu ya Mercedes, na Fernando Alonso kutoka Uhispania, na wa timu ya Ferrari.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Dereva kutoka Australia Webber aliweza kuongoza mashindano ya Monte Carlo kuanzia mwanzo hadi mwisho

Webber, dereva wa Red Bull, aliongoza mashindano hayo kutoka mwanzo hadi mwisho.

Dereva wa McLaren, Lewis Hamilton wa Uingereza, kuna wakati aliweza kujikita katika nafasi ya tatu, lakini akapitwa na dereva wa Ferrari Alonso, na vile vile Sebastian Vettel wa Red Bull, ambao walitumia mbinu bora za kuhakikisha walidumisha kasi yao na kumpita.

Wakati mmoja Alonso maksudi alibaki nyuma, ili kuokoa magurudumu yake, na ili yaweza kunasa barabara vyema katika dakika za mwishomwisho alipohitaji kasi kabla ya kuvifikia vituo vya kupata huduma ya gari kurekebishwa.

Mbinu hiyo hatimaye ilimsaidia kufanya vyema, kwani Webber na Hamilton waliposimama katika raundi ya 29, raundi mbili zaidi ya Rosberg, Alonso aliweza kwenda mzunguko mmoja zaidi, na akienda kwa kasi sana wakati huo.

Mbinu hiyo ilimwezesha kumtangulia Hamilton.

Dereva mwingine wa Uingereza, na wa timu ya McLaren, Jenson Button, alipata mashindano hayo kuwa magumu, na baada ya muda mfupi alilazimika kuondoka mapema.

Ushindi wa Mark Webber umeandikisha historia mpya katika mashindano ya Formula 1, kwa kuwa ni mara ya kwanza madereva sita tofauti kuibuka washindi baada ya mashindano sita ya msimu.

"Ninahisi nimefanikiwa kufanya maajabu," alielezea Webber kutoka Australia.”

"Ni siku ya ajabu kwa timu na mimi binafsi, na nimefurahi sana kupata tena ushindi hapa.”

Kufuatia matokeo hayo, Alonso wa timu ya Ferrari sasa anaongoza katika kuwania ubingwa wa dunia, akimtangulia Vettel na Webber kwa pointi tatu.

Hamilton anateremka kutoka nafasi ya tatu hadi nne, akiachwa nyuma na Alonso kwa pointi 13.