Dirk Kuyt ahama Liverpool

Mchezaji wa safu ya mbele ya Uhalonza Dirk Kuyt ameihama klabu ya Liverpool na kujiunga na Fenerbahce ya Uturuki kwa mkataba wa miaka mitatu. Mshambuliaji huyo anaihama Liverpool baada ya kipindi cha miaka sita.

Kuyt mwenye umri wa miaka 31 alihamia uwanja wa Anfield mnamo mwaka 2006 na kushiriki mara 250 akifunga jumla ya mabao 71.

Taarifa ya Liverpool iliyotolewa kufuatia hatua hio imesema kua Kila mmoja anamtakia Dirk kila la heri na kumshukuru kwa mchango wake.

Aliposajiliwa, Kuyt alisema wakati huo, Kwangu mimi, Liverpool ni ndoto iliyokamilika. Hapana cha kuilinganisha nayo klabu hii, yenye sifa na historia ya kujivunia, alisema.

Mechi yake ya kwanza kushiriki ilikua dhidi ya West Ham United mwezi Agosti mwaka 2006, alipoingia kuchukua mahala pa Peter Crouch ambapo upande wake uliondoka na ushindi wa 2-1.

Bao lake la kwanza lilipatikana mwezi mmoja baadaye alipofunga bao la kwanza katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Newcastle.

Baadaye alipendwa na mashabiki wa Liverpool, kivutio kikiwa mchangon wake katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Everton kwenye uwanja wa Goodison Park mwaka 2007 kisha alipofunga 3- peke yake dhidi ya Manchester United, mahasimu wakuu wa klabu kutoka Anfield.

Kuyt ambaye ameshiriki mara 80 kwa Timu yake ya Taifa ya Uholanzi, pia alifunga dhidi ya AC Milan katika mchuano wa Ligi ya mabingwa mwezi Mayi mwaka 2007.

Msimu uliopita mshambuliaji huyo alipata shida kupata nafasi katika kikosi kikuu, akishiriki mara 22 pekee na kuletwa kama mchezaji wa ziada mara tano katika mechi tisa za mwisho wa msimu.

Kwa wakati huu mchezaji huyo aliyesajiliwa kutoka klabu ya Utrecht yuko pamoja na wenzake wa Timu ya Taifa ya Uholanzi wakijinoa kwa ajili ya michuano ya Ulaya 2012 ambapo Wadachi watachuana na Denmark katika mechi yao ya ufunguzi jumamosi ijayo.