Michuano ya Kombe la Dunia Afrika

Wawakilishi wa mara sita wa Bara la Afrika kwenye fainali za Kombe la Dunia Cameroon walisahau yaliyopita ya kukosa kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kuichapa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mjini Kinshasa.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Michuano ya kufuzu kombe la Dunia

Senegal na Algeria -zilizowahi kuiwakilisha Afrika zilikua miongoni mwa timu zilizoanza vizuri kwa ushindi.

KUNDI F Matumaini ya Kenya kushiriki kombe la Dunia kwa mara ya kwanza yalididimizwa na sare ya kutofungana dhidi ya Malawi nyumbani kwao mjini Nairobi. Timu ya Harambee stars ilikua na kibarua katika kujaribu kuvunja ngome ya Malawi na mkufunzi wa Malawi, Kinnah Phiri alisema baada ya mechi hio kua Kenya itakua na wakati mgumu kufuzu hilo likidhihirishwa na jinsi ilivyoshindwa kutumia vizuri uwanja wa nyumbani.

Mechi nyingine ya kundi hili imepangwa kuchezwa huko Calabar ambako Nigeria inaipokea Namibia jumapili.

KUNDI G Kufuatia ushindi wa Misri wa 2-0 dhidi ya Msumbiji mnamo siku ya Ijumaa, timu za Zimbabwe na Guinea zinafahamu vyema kua zitahitaji ushindi mkubwa jumapili.

KUNDI H Katika Kundi hili Algeria ilijiwekea matumaini makubwa kwa ushindi mkubwa kwa kuikandika Rwanda 4-0 mjini Blida.

Wafungaji wa Algeria walitanguliwa na bao la Sofiane Feghouli kabla ya El Arabi Soudani kufunga mawili na Islam Sliani kumalizia udhia na la nne.

Benin na Mali zimepangiwa kuchuana mjini Cotonou jumapili.

KUNDI I Cameroon ilianza kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mjini Yaounde. Mfungaji wa bao la Cameroon alikua Eric Choupo-Moting kupitia mkwaju wa peneti.

Mechi ya pili ya kundi hili ni Togo inayoipokea Libya.

KUNDI J Senegal ilishtushwa kwa bao la haraka nyumbani na Liberia lakini ikabadili hali ya mambo kwa kuondoka na ushindi wa 3-1 chini ya Kocha wake mpya Joseph Koto.

Koto aliteuliwa kama Kocha wa Senegal baada ya Mfaransa Pierre Lechantre kujiondoa.

Mechi nyingine ya kundi hili ni Angola iliyoshiriki fainali ya Kombe la Dunia la mwaka 2006 ikiipokea Uganda mjini Luanda.