Ufaransa haitutishi!

Mchezaji wa timu ya soka ya taifa ya England, Stewart Downing, amesema kamwe hawana wasiwasi watakapopambana na Ufaransa katika michuano ya Euro 2012.

Image caption Downing anasema England haitishwi na wachezaji wa Ufaransa

Downing amesema kikosi cha England kamwe hakitababaika wakati watakapokutana na Ufaransa siku ya Jumatatu.

Meneja Roy Hodgson ataiongoza England katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Ufaransa, kabla ya kucheza na Sweden tarehe 15 Juni, na siku nne baadaye, kupambana na wenyeji Ukraine.

Downing, mwenye umri wa miaka 27, amesema: "Tuna imani kwamba tutapata matokeo mazuri. Hatuwaogopi."

"Tunajua timu yao ni nzuri, lakini hata sisi hucheza vizuri. Tunazifahamu nguvu zao na vile vile udhaifu."

Alikanusha kwamba wachezaji wa England wamekuwa wakizungumza kuhusu mchezaji wa Manchester United, Rio Ferdinand, kwa kuachwa nje ya kikosi hicho.

"Yeyote meneja atakayemchagua tunaweza kuendelea naye. Mimi najitahidi zaidi kuangazia nafasi ninayocheza, na wenzangu katika timu wanafanya vivyo hivyo."

Downing ni kati ya wachezaji sita wa klabu ya Liverpool katika timu ya taifa ya England.

Timu hiyo ina wachezaji wengi zaidi katika timu ya taifa kuishinda klabu yoyote nchini England, licha ya klabu kumaliza katika nafasi ya nane katika ligi kuu ya Premier.

Downing, ambay zamani aliichezea Middlesbrough na Aston Villa kama kiungo wa kati, aliitetea klabu yake ya Liverpool: "Ikiwa utaangalia namna tulivyocheza, tuliweza kuzishinda vibaya timu wakati mwingine, lakini tulishindwa kupata nguvu katika kumalizia ligi."