Poland yakabwa na Ugiriki

Mashabiki wa Poland
Image caption Mashabiki wa Poland

Mashindano ya mchezo wa mpira wa miguu ya Mataifa ya Ulaya, Euro 2012 yameanza rasmi nchini Poland, moja ya nchi zinazoshirikiana kuandaa mashindano ya mwaka huu.

Katika mechi ya ufunguzi Dimitris Salpigidis alirudisha bao katika kipindi cha pili kusawazisha bao la mwenyeji wake Poland lililopatikana katika kipindi cha kwanza.

Mshambuliaji huyo aliwaudhi mashabiki wa Poland waliotazamia kuanza mashindano waliyoyaandaa wenyewe kwa kutikisa nyavu za Poland katika dakika ya 51, dakika 6 baada ya kipindi cha pili kuanza.

Hadi mapumziko, Robert Lewandowski anayetazamiwa kujiunga na Klabu ya Ligi ya England, Manchester united msimu ujao alikua ameisha ipatia Poland bao la kwanza katika dakika ya 17 ya mchezo.

Timu hizi mbili zilimaliza mechi zikiwa na wachezaji 10 kila upande na Ugiriki itajilaumu kwa kupoteza fursa wazi ya kuongoza kupitia mkwaju wa peneti baada ya Giorgos Karagounis kukosa peneti hio kufuatia kosa la kipa wa Poland Wojciech Szczesny kusababisha aondolewe kwa kadi nyekundu kwa kumuangusha Salpigidis katika eneo la hatari mnamo dakika ya 69th.

Kabla ya hapo beki wa Ugiriki Sokratis Papastathopoulos alikua mchezaji wa kwanza kwenye mashindano haya ya Euro kuonyeshwa kadi nyekundu, baada ya kupokea kadi mbili za njano mnamo dakika ya 35 na 44.

Hivi sasa timu hizi zina pointi 1 kila moja.