Urusi haina huruma na Czech

Urusi na Czech Haki miliki ya picha AFP
Image caption Urusi imethibitisha katika mechi yao ya kwanza ya Euro 2012 kwamba ina mchezo wa kuburudisha

Urusi ilionyesha ustadi mkubwa ilipocheza na Jamhuri ya Czech katika mechi ya pili ya Euro 2012 siku ya Ijumaa, na mabao mawili ya Alan Dzagoev kuisaidia kuwaangamiza wapinzani wao katika siku ya kwanza ya mashindano hayo.

Dzagoev aliiwezesha Urusi kupata bao la kwanza, huku Roman Shirokov akiandikisha la pili, baada ya Andrey Arshavin kumuandalia mpira huo.

Vaclav Pilar aliweza kuifungia Jamhuri ya Czech bao moja, na kupunguza tofauti ya mabao kati ya timu hizo mbili.

Lakini ilielekea kana kwamba bao hilo la Czech liliamsha gadhabu za Warusi, na ambao pasipo kusubiri sana, Dzagoev aliweza kutumbukiza magoli mawili zaidi, na mchezaji wa zamu Roman Pavlyuchenko naye akiandikisha lake pia.

Ilikuwa dhahiri kwamba Urusi ndio iliyokuwa timu bora katika uwanja wa Wroclaw, na Jamhuri ya Czech ikionyesha udhaifu mkubwa nchini Poland.

Kocha wa Czech, Michel Bilek bila shaka atakuwa na kibarua kigumu katika kuwahimiza wachezaji wake waliovunjika moyo kwamba bado wanaweza kujikakamua na kufanya vyema watakapokutana na Ugiriki tarehe 12 Juni.

Hii itakuwa ni mechi muhimu kwa Czech, ikiwa ina nia ya kuendelea na mashindano ya Euro.

Kutokana na wenyeji Poland kumaliza mechi ya ufunguzi dhidi ya Ugiriki kwa sare ya 1-1, timu ya Urusi na Czech walianza mechi yao wakifahamu kwamba mshindi katika pambano lao ataweza kuwa kileleni katika kundi lao.

Urusi, ambao chini ya meneja Guus Hiddink waliweza kufika nusu fainali katika mashindano ya mwaka 2008, na kuonyesha kwamba hawana utani katika michuano ya mwaka huu.