Jamhuri ya Ireland yakata tamaa

Matumaini ya Jamhuri ya Ireland kuvuka hatua ya makundi katika mashindano ya Euro 2012 yalididimia, baada ya kulazwa magoli 3-1 na Croatia katika mji wa Poznan, Poland.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Meneja Giovanni Trapatton bila shaka atahitaji juhudi za ziada kuimarisha mchezo wa Jamhuri ya Ireland

Mario Mandzukic aliweza kufunga kwa kichwa, huku juhudi za kipa Shay Given kuuzia mpira huo zikikosa kufua dafu.

Lakini juhudi za wachezaji wa Jamhuri ya Ireland hatimaye zilifanikiwa, wakati Sean St Ledger aliposawazisha.

Hata hivyo, kabla kipenge cha kukamilisha nusu ya kwanza ya mchezo, Nikica Jelavic alibadilisha matokeo, na kuiwezesha Croatia kuongoza 2-1.

Mandzukic aliweza kuandikisha bao la tatu, ambalo mpira uliingia wavuni ukisindikizwa kimakosa na kipa wa Given.

Jamhuri ya Ireland haiwezi kulalamika sana kuhusiana na matokeo ya mechi hiyo, kwani ilikuwa wazi timu yao bado haijajiandaa vyema.

Kabla ya mechi, mashabiki wengi kutoka Jamhuri ya Ireland walikuwa na matumaini ya kufanya vyema katika mechi hiyo ya kundi C, lakini uwanjani ilikuwa ni wazi kwamba Croatia ndio timu bora, meneja wao mzoefu, Giovanni Trapattoni, bila shaka itambidi kufanya kazi ya ziada ikiwa Jamhuri ya Ireland itaepuka fedheha katika mashindano hayo.