Italia yaibana Uhispania

Italia ilitangulia bao
Image caption Italia ilitangulia bao

Mabingwa wa Dunia Uhispania imeanza utetezi wa Kombe lao la ubingwa wa mashindano ya Ulaya kwa sare ya 1-1 dhidi ya Italia katika pambano la kundi C mjini Gdansk.

Italia ndiyo iliyotangulia baada ya kipindi cha kwanza kumalizika bila bao lolote kufungwa na alikua Antonio Di Natale aliyeingia badala ya Balloteli kufunga bao katika dakika ya 60.

Dakika nne baadaye Mabingwa wa Dunia na Ulaya walifumania lango la Italia na licha ya juhudi na umahiri wa Mabeki David Silva alimuona Cesc Fabregas na kumuwekea pasi maridhawa na bila kufanya makosa akaupenyeza mpira kumpita goli wa Italia Buffon.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Italia yachacha na Uhispania

Matokeo hayo yanaliweka kundi la C wazi ambapo Italia na Uhispania zinaondoka zote zikiwa na pointi moja.

Kabla ya mashindano haya wadadisi walionelea kama Uhispania itakabiliwa na kibarua kigumu kutetea taji lake kutokana na wachezaji wake wengi kuwa wachofu mno. Jumla ya wachezaji 23 wa timu hii ya Taifa wamecheza jumla ya dakika 89,884 katika msimu uliopita ikilinganishwa na wenzao walioshiriki kwa upungufu wa dakika 17,000.

Timu mbili zilizomo kwenye kundi la C Jamhuri ya Ireland na Croatia lazima zimeridhishwa na matokeo haya zikiona kua na fursa ya kufanya vyema na uwezekano mkubwa wa kufuzu kutoka michuano ya makundi.