Wenyeji Poland wajizatiti

Wenyeji Poland walionyesha mchezo wa hali ya juu katika uwanja wa Warsaw dhidi ya Urusi, mechi iliyokwisha kwa sare ya 1-1.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Poland imejiongezea matumaini ya kuvuka salama mechi za makundi

Hii ilikuwa ni mechi ya pili siku ya Jumanne.

Kwa sare hiyo, Poland ina matumaini kwamba huenda ikavuka mechi za makundi.

Poland, ambayo inashirikiana na Ukraine katika kuandaa mashindano ya Euro 2012, tayari ilikuwa imelemewa bao 1-0 kabla ya kufanikiwa kusawazisha, kupitia nahodha Jakub Blaszczykowski katika kipindi cha pili, na kwa mkwaju wa mguu wa kushoto.

Urusi walikuwa wamefanikiwa kuongoza walipopata bao katika dakika ya 37, kupitia mshambulizi hodari Alan Dzagoev baada ya kupigiwa pasi safi na Andrey Arshavin.

Timu zote zilionyesha mchezo wa hali ya juu, na kulikuwa na uwezekano wa kila timu kujipatia ushindi.

Matokeo hayo yanamaanisha ushindani ni wazi katika kundi A, na kimahesabu timu zote nne katika kundi hilo zinaweza kufuzu kuingia robo fainali.

Kabla ya mechi hiyo, mashabiki wa Urusi walikuwa tayari wamewaudhi wenyeji Poland katika mji mkuu wa Warsaw.

Mashabiki wa Urusi, katika kuadhimisha siku kuu ya uhuru wao, waliendeleza sherehe zao katika barabara za Warsaw, jambo ambalo liliwaudhi wenyeji, na kuwafanya polisi wa kutuliza ghasia kuingilia kati na kujitahidi kuwatawanya mashabiki wa pande zote mbili.