Ureno yaponyoka aibu

Pepe afunga bao la Ureno Haki miliki ya picha AFP
Image caption Pepe afunga bao

Ureno yaichapa Denmark 3-2 katika mchuano wa kundi B katika michuano ya Euro 2012.

Ushindi wa Ureno wa 3-2 dhidi ya Denmark katika michuano wa Euro 2012 unaweka matumaini ya nchi hiyo kuendelea hadi robo fainali.

Bao lililonusuru matumaini hayo lilitiwa kimyani na Silvestre Varela aliyeletwa kipindi cha pili aliyefunga bao na kufuta bao la Nicklas Bendtner la kusawazisha mapema katika kipindi cha pili.

Ureno iliongoza kupitia kipindi cha kwanza kupitia wachezaji wasiotarajiwa ambapo beki Pepe na Helder Postiga waliipatia Ureno mabao ya kuwapa matumaini ya kupiga hatua.

Lakini kukosa fursa kadhaa kwa nyota wao Cristiano Ronaldo kulitishia kuiangusha Ureno na kurejea nyumbani mapema.

Ushindi huu unaiweka Ureno sambamba na Denmark kwa pointi kutokana na ushindi wa Denmark dhidi ya Uholanzi katika mechi ya ufunguzi kwa pande hizo mbili.

Katika mchezo wa pili siku ya Jumatano, Mario Gomez wa Ujerumani aliwafunza wachezaji wa Uholanzi namna ya kufunga mabao, walipoondoka na ushindi wa magoli 2-1.

Mshambulizi huyo wa Bayern Munich kwa upesi aliweza kugeuka alipopokea mpira kutoka kwa Bastian Schweinsteiger na kuandikisha bao la kwanza la Ujerumani katika dakika ya 24, na baadaye kuongezea la pili katika dakika ya 38, katika kuhakikisha Uholanzi itaondoka katika michuano ya Euro 2012 mapema.

Robin van Persie, ambaye alishindwa kuitumia nafasi nzuri iliyojitokeza na kuiwezesha Uholanzi kuongoza kufunga, hatimaye aliwafungia bao la kujituliza, lakini timu yake ikashindwa kufunga magoli zaidi.