Balotelli alaumiwa kwa sare na Croatia

Balotelli Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mario Balotelli

Jina la Mario lilitajwa na kusababisha furaha kwa mmoja wa Mameneja wa Timu zilizokua uwanjani kwa mchuano wa kundi C kati ya Italia na Croatia.

Ni jina la mshambuliaji Mario Mandzukic aliyefunga bao la Croatia mnamo dakika ya 72 kutumia fursa pekee kurudisha bao la Italia, lakini Mario mwenzake katika jezi za bluu hakufua dafu na hakuonyesha sababu za imani ya Meneja wake kuamini kua anaweza kubadilika.

Mshambuliaji huyu anayechezea klabu ya Manchester City na mwenye kipato kikubwa cha mshahara kuliko wa Mandzukic na labda magari kadhaa ya fahari, angetazamiwa kuwasha michuano ya mwaka 2012.

Badala ya kuonyesha jitihada Balotelli anaonekana kama mtu aliyechoka na kutohusika na yanayoendelea uwanjani licha ya uwezekano wa kukosa kuingia robo fainali umeanza kuonekana.

Tafauti na Mandzukic anatumia mabavu kupasua ngome na kuonyesha nia na tamaa yake ya kuiona Timu yake ikiondoka na heshima.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Balotelli

Mandzuk alifunga mabao dhidi ya Ireland katika mechi ya kwanza Croatia ilipoizima Ireland 3-1 akifuatisha bao la kunyemelea kuisumbua Italia.

Ni mchezaji asiyejulikana nje ya Bundesliga ya Ujerumani mbali na mashabiki wa VfL Wolfsburg. Na haitostaajabisha wengi endapo katika wiki chache zijazo akianza kupokea maombi ya kujiunga na vilabu maarufu na vikuu barani Ulaya.

Wadadisi wanasema kua sababu ya Italia kushindwa kuizima Croatia ni Balotelli na hivyo kumaliza mchuano huo kwa Italia 1 Croatia 1.