Jamhuri ya Ireland nje!

Uhispania na Ireland Haki miliki ya picha Reutres
Image caption Jamhuri ya Ireland imeondolewa kutoka Euro 2012 kwa urahisi

Fernando Torres alifanikiwa kutumbukiza magoli mawili wavuni katika mechi ambayo Uhispania kwa urahisi ilifanikiwa kuilazimisha Jamhuri ya Ireland kukusanya virago na kuondoka katika mashindano ya Euro 2012.

Mkwaju wa Torres uliopigwa kwa kasi mno kutoka yadi kumi ulianzisha mfululizo wa magoli, mara tu baada ya bao hilo la kwanza kuingia wavuni katika dakika ya nne ya mchezo.

Mara tu baada ya kipindi cha pili, David Silva aliongezea bao la pili katika dakika ya 49.

Torres alifanikiwa kuongezea bao lake la pili katika mechi hiyo katika dakika ya 70, huku mchezaji wa zamu Cesc Fabregas naye akiandikisha bao la nne na la kufunga kazi katika ya 83.

Matokeo hayo yameiwezesha Uhispania kuipita Croatia na kuongoza kundi C.

Uhispania sasa itakutana na Croatia siku ya Jumatatu, mechi ambayo inatazamiwa kuwa ngumu.

Mchezo wa Jamhuri ya Ireland bila shaka ulikuwa na dosari nyingi, na katika mashindano yao makubwa baada ya kipindi cha miaka kumi, wamefungwa magoli mengi kirahisi.

Katika kila mechi waliocheza ya Euro 2012, katika kila nusu ya mchezo ilipoanza, walifungwa bao chini ya dakika nne za mwanzo, hii ikiwa ni pamoja na katika mechi walioshindwa na Croatia magoli 3-1.

Kabla ya mech hiyo, Jamhuri ya Ireland ilikuwa haijawahi kushindwa zaidi ya magoli matatu katika mashindano makubwa.

Lakini hayo sasa yametokea, wakifungwa magoli mengi mara mbili katika kipindi cha siku tano.

Kwa Uhispania ambayo ilitoka sare ya 1-1 iipocheza na Italia katika mechi yao ya kwanza, hili ni onyo muhimu kwa wapinzani, kuonyesha kwamba nchi hiyo ina nia ya kuandikisha historia kwa kuwa mabingwa katika mashindano makubwa.

Ujumbe umewasilishwa kikamilifu chini ya saa 24 tangu Ujerumani nayo ilipoonyesha uhodari wake kwa kuilaza Uholanzi magoli 2-1.