Ureno nusu fainali Euro 2012

Ronaldo Haki miliki ya picha Getty
Image caption Bao moja la Ronaldo limeiwezesha Ureno kuifunga Czech na kuingia nusu fainali Euro 2012

Mshambulizi Cristiano Ronaldo aliwaridhisha mashabiki wa Ureno kwa kucheza vizuri sana usiku wa Alhamisi, na juhudi zake kuiwezesha nchi yake kuishinda Jamhuri ya Czech bao 1-0 katika mechi ya mwanzo ya robo fainali ya Euro 2012, na kufanikiwa kuifikisha hadi nusu fainali.

Ronaldo, ambaye alifunga magoli mawili wakati katika mechi ya awali ya mashindano hayo nchi yako ilipocheza na Uholanzi, aliweza kugonga mwamba katika nusu ya kwanza na ya pili katika mechi dhidi ya Jamhuri ya Czech.

Hatimaye aliweza kuuelekeza mpira hadi wavuni kwa kichwa, huku zikiwa zimesalia dakika 12 kabla ya mechi kumalizika, na kipa Petr Cech akiweza kuufikia mpira, lakini hakuweza kuuzuia kutokana na nguvu nyingi zilizotumiwa na Ronaldo.

Ilikuwa dhahiri kwamba wachezaji wa Czech waliingia uwanjani wakiwa na nia ya kuimarisha ngome yao, na wala sio kushambulia, na kamwe hawakumtisha kabisa kipa wa Ureno.

Ureno sasa itakutana aidha na Uhispania au Ufaransa katika juhudi za kufuzu kwa fainali.

Bila shaka timu ambayo itakutana na Ureno itakuwa na wasiwasi ni vipi itaweza kumzuia Ronaldo, ambaye baadhi ya wadau wa soka wanasema kwa sasa ndiye mchezaji bora zaidi barani Ulaya.