Kvitova na Serena wafuzu raundi ya nne

Petra Kvitova Haki miliki ya picha AFP
Image caption Petra Kvitova amefuzu kuingia raundi ya nne

Bingwa mtetezi wa mashindano ya Wimbledon kwa upande wa kina dada, Petra Kvitova kutoka Jamhuri ya Czech, na bingwa mara nne katika mashindano hayo, Mmarekani Serena Williams, wote walifuzu kuingia raundi ya nne ya mashidano hayo siku ya Jumamosi.

Williams, baada ya kulemewa na mpinzani kutoka Uchina, Zhenj Jie, hatimaye aliweza kupata ushindi wa 6-7 (5-7) 6-2 9-7

Kvitova alimshinda kwa urahisi mpinzani wake kutoka Marekani, Varvara Lepchenko, kwa 6-1 6-0.

Ana Ivanovic, ambaye amepangwa katika nafasi ya 14 katika orodha ya wachezaji bora wa kike katika mashindano ya Wimbledon, aliweza kumshinda Mjerumani Julia Goerges 3-6 6-3 6-4, na sasa atakutana na mchezaji aliyepangwa katika nafasi ya pili katika mashindano hayo, Victoria Azarenka kutoka Australia.

Yaroslava Shvedova alikuwa mchezaji wa kwanza kupata ushindi wa kirahisi na kufuzu moja kwa moja kusonga mbele, baada ya mpinzani wake, Sara Eerrani kushindwa kupata pointi katika seti ya mwanzo, na hatimaye kushindwa 6-0 6-4.

Shvedova, aliyepangwa katika nafasi ya 65 ya mashindano hayo, sasa lazima ajiandae vyema kwa raundi ya nne, katika kukutana na Serena, aliyepangwa katika nafasi ya 6 katika mashindano ya mwaka huu ya Wimbledon.