Murray amshinda Baghdatis

Andy Murray Haki miliki ya picha AP
Image caption Murray alishinda katika pambano walilocheza kwa haraka baada ya kutambua kwamba pambano litaendelea hata baada ya saa tano usiku za Uingereza

Andy Murray, mchezaji wa Uingereza, aliwafurahisha mashabiki wa nyumbani katika uwanja wa Wimbledon, raundi ya tatu siku ya Jumamosi, wakati alipofanikiwa kumshinda mpinzani wake kutoka Cyprus, Marcos Baghdatis, katika pambano ambalo lilikwisha saa tano na dakika mbili za London, sawa na saa saba na dakika mbili usiku, saa za Afrika Mashariki.

Hili ndilo pambano ambalo lilikwisha usiku zaidi katika historia ya Wimbledon, na wachezaji wote wawili hawakufahamu kama wataweza kuendelea kadri muda ulivyozidi kuendelea.

Murray, aliyepangwa katika nafasi ya nne katika orodha ya wachezaji bora zaidi katika mashindano ya Wimbledon mwaka huu, aliweza kumshinda Baghdatis kwa 7-5 3-6 7-5 6-1 katika muda wa saa tatu na dakika 13.

Sheria za Wimbledon ni kwamba mchezo haupaswi kuendelea baada ya saa tano usiku kwa saa za Uingereza, na Murray na Baghdatis inaelekea waliongeza kasi ya mchezo ili kukamilisha pambano lao haraka.

Hata hivyo lilikuwa pambano la kuridhisha mno, sio tu kwa mashabiki wa nyumbani Uingereza, bali pia kwa mamilioni ya wapenda tennis kote ulimwenguni.

Mapambano mengine ambayo yamechezwa usiku mwaka huu katika uwanja wa Wimbledon na yaliyokuwa ya kusisimua ni pamoja na yale yaliyowahusisha wachezaji Novak Djokovic, Rafael Nadal na Roger Federer.

Murray sasa atapumzika Jumapili, lakini Jumatatu ana kibarua cha kupambana na Marin Cilic katika pambano la raundi ya nne.