Wimbledon

Serena Williams Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Huenda siku ya Jumamosi akaifikia rekodi ya dadake Venus Williams ya kuibuka mshindi wa Wimbledon mara tano

Serena Williams amejiongezea matumaini ya kuibuka bingwa wa mashindano ya Wimbledon kwa kina dada kwa mara ya tano, baada ya kufuzu kupambana katika fainali, baada ya kumshinda Victoria Azarenka kutoka Urusi katika seti zote.

Mchezaji huyo wa Marekani alimshinda mpinzani wake kwa urahisi, kwa 6-3 7-6 (8-6), na sasa atapambana na mchezaji kutoka Poland katika fainali, Agnieszka Radwanska.

Radwanska, ambaye amepangwa katika nafasi ya tatu katika orodha ya wachezaji bora zaidi wa kike katika mashindano ya Wimbledon mwaka huu, naye kufuzu kwa fainali aliweza kumuondoa Angelique Kerber kutoka Ujerumani kwa kumshinda 6-3 6-4.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Radwanska kucheza katika fainali ya mashindano makubwa ya tennis, kiwango cha Grand Slam.

"Ni mchezaji wa ajabu. Anacheza vizuri sana," alielezea Williams kuhusu mchezo wa Radwanska.

Radwanska, mwanamke wa kwanza kuingia fainali ya mashindano makubwa ya Grand Slam katika kipindi cha miaka 75, alicheza vizuri katika pambano lake, lakini katika historia ya kupambana na Williams, kamwe hajawahi kumshinda hata katika seti moja.

Walipokutana katika mapambano ya mawili mara ya mwisho, ikiwa ni pamoja na robo fainali ya Wimbledon ya mwaka 2008, Williams alimshinda kwa urahisi.

Iwapo Serena Williams ataibuka mshindi katika fainali ya Jumamosi, basi ataifikia rekodi ya dadake Venus, ya kuwa mshindi mara tano katika mapambano ya Wimbledon.

Kwa jumla, atakuwa amepata ubingwa wa mashindano 14 ya Grand Slam.