Danny Garcia bingwa wa WBA na WBC

Amir Khan Haki miliki ya picha 1
Image caption Amir Khan

Majaliwa ya mwanamasumbwi wa Uingereza Amir Khan yamefika njia panda baada ya kutandikwa na kijana chipukizi katika masumbwi Danny Garcia wa Marekani akishikilia taji la WBC. Garcia bila kutarajiwa alimnyuka bingwa wa taji la WBA katika raundi ya nne na kuendeleza sifa yake ya kutoshindwa tangu kuanza mchezo wa masumbwi ya kulipwa.

Licha ya kushindwa mapema katika mchezo, Khan alimjeruhi Garcia kunako raundi ya pili akionekana kudhibiti mchezo vizuri raundi zote mbili.

Lakini Garcia alibadilika katika raundi ya tatu na zikisalia sekunde chache kabla ya kipenga cha mapumziko, Khan alishangaa kuona mgongo umenyooka kwenye sakafu baada ya konde lililomponda nyuma ya sikio la upande wa kulia. Baada ya hapo ikawa ni mshike mshike, Khan akitafuta kimbilio hadi kipenga kilipopigwa kumnusuru makonde ya mfululizo.

Mwanzoni mwa raundi ya nne, Khan alionekana kupunguza vimulimuli vilivyomzonga mapema kwa makonde ya Garcia lakini alidondoshwa tena kwa konde la Garcia la mkono wa kushoto ulioonekana kumgusa utosi na kumgaragaza chini akakaa kitako.

Ingawaje Khan aliinuka na kurusha makonde yake mazito, mkono wa kushoto wa Garcia ulikipata kichwa cha Khan na kurejesha chini. Aliweza kusimama ingawa miguu ilionekana kama isiyoweza kunyooka kumwezesha kuhimili makonde mazito ya mpinzani wake.

Refa wa mchuano huo Bayless alichukuwa uwamuzi baada ya kumtazama usoni kwa makini na macho yaliyoonekana kuchoka akaamuwa pambano liishie hapo.

Ni hivi karibuni tu Amir Khan karejeshewa mikanda yake baada ya Lamont Peterson wa Marekani kupatikana kua alitumia dawa ya kuongezea nguvu mwili.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Khan akichapwa pambano la zamani kidogo

Baada ya pambano, Khan alisema haikuwa bahati yangu usiku huu.

Garcia kwa upande wake ulikuwa usiku wa furaha na sherehe baada ya kushinda mikanda yote miwili, WBC na WBA akizidi kuimarisha rekodi yake ya ushindi wa mapambano 24 bila kupoteza pamoja na ushindi wa mara 15 kwa knock out. Khan ameshiriki michuano 26 kashindwa mara tatu ingawa amewahi kushinda 18 kwa kuwakwaza wapinzani wake.

Amir Khan alisema atainuka na kurudi ulingoni na kutaraji kuwa Garcia atawapa fursa ya pambano la marudiano nchini Uingereza. Lakini Babake Garcia hakusita kupinga ombi la Khan kwa kusema, 'khan alimdharau sana mwanangu, kwanini tumpe fursa, ya nini? Hatuwezi kumpa fursa kama hiyo, alisema mzee Angel Garcia.