Havalange kuvuliwa heshima

Haki miliki ya picha AP
Image caption Havalange alitawala soka miaka 40

Rais wa FIFA Sepp Blatter amethibitisha nia yake ya kuzidisha juhudi za kumuondoa aliyekuwa Rais wa shirika hilo Joao Havalange kwenye uwanachama wa FIFA.

Havelange, mwenye umri wa miaka 96 pamoja na aliyekuwa mkwe wake Ricardo Teixeira walitajwa katika hati za mahakama hivi karibuni kuwa walipokea mlungula kutoka kwa kampuni mshirika wa FIFA -ISL iliyofilisika katika miaka ya 1990.

Ingawa alisema awali kuwa hakuwa na uwezo wa kuwachukulia hatua yoyote, Rais wa sasa Blatter hivi sasa atajitahidi kuona kwamba Havalange anavuliwa hadhi ya uwanachama wa FIFA.

Ameliambia gazeti la nchini Uswizi SonntagsBlick: " Havelange ni milioneya wa kupindukia. Ni jambo la kushangaza kuona kua alikubali na kupokea mlungula.Hana mahitaji ya kutapatapa hivyo.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ricardo Teixeira

Nitapendekeza kwa kamati ya utendaji suala hili lishughulikiwe kwenye kikao chetu kinachokuja. Lazima aondolewe,haiwezekani asalie kuwa na heshima ya Rais asiye na madaraka ya utendaji alisema Blatter.

Wababe hao wawili, Havalange na Teixeira hawakuwahi kuchukuliwa hatua yoyote ya kinidhamu na FIFA. Badala yake shirika hilo lilikubalia kuilipa koti faranga za uswizi milioni 2.5 kama fidia kwa sharti kwamba kesi dhidi ya Havalange na Teixeira isiendelee na itupwe nje ya mahakama.

Taarifa ya koti inasema kuwa Havalange kwa uchache alipokea faranga milioni 1.5 Teixeira akapokea faranga milioni 12.74 sawa na dola za Marekani milioni 8.37 na kwa pamoja huenda walipokea faranga milioni 21.9.