Azam yaingia robo fanali Kombe la Cecafa

Timu changa na mpya kwenye mashindano ya soka Afrika Mashariki na Kati Azam ya Tanzania imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya Cecafa.

Azam, iliyomaliza ligi ya Tanzania msimu uliopita ikiwa nafasi ya pili, ilisajiliwa Ligi Kuu ya Vodacom mwaka 2007 na inamilikiwa na tajiri mwenye viwanda nchini Tanzania, Salim Bakhresa.

Azam ilifuzu kutoka Kundi C baada ya kutoka suluhu ya kutofungana na Tusker ya Kenya. Mafunzo nayo ilifuzu kutoka Kundi hilo, huku Tusker wakitupwa nje ya mashindano.

Timu nyingine ambazo zimeingia robo fainali ni bingwa mtetezi Yanga ya Tanzania na mahasimu wao Simba.

Vita Club kutoka DR Congo, URA kutoka Uganda, APR ya Rwanda na Atletico ya Burundi ndizo timu nyingine zilizofanikiwa kutinga nane bora.

Mechi za robo fainali zitachezwa Jumatatu na Jumanne. Mechi za Jumatatu zitakuwa kati ya APR na URA na Yanga dhidi ya Mafunzo. Simba watacheza na Azam na Vita Club watacheza na Atletico Jumanne.

Mbali na Tusker, timu nyingine zilizoaga mashindano baada ya mzunguko wa makundi ni Al Salaam Wau ya Sudan Kusini na Ports ya Djibouti.

Mshindi wa mashindano atazawadiwa dola 30,000 huku mshindi wa pili na tatu wakipata dola 20,000 and 10,000.

Fedha zitatolewa na Rais wa Rwanda Paul Kagame, ambaye mashindano haya yamepewa jina lake.