Azam yaingia fainali

Timu ya Azam
Image caption Kocha Stewart Hall na baadhi ya wachezaji wa Azam

Timu mpya kwenye mashindano ya klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam ya Tanzania, na vile vile mabingwa watetezi Yanga, zimeingia fainali ya michuano hiyo ya Cecafa.

Azam imetinga fainali baada ya kuifunga Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo 2-1, wakati Yanga wamepenya baada ya kuilaza APR ya Rwanda 1-0 kwenye mechi zilizochezwa Alhamisi mjini Dar es Salaam.

Vita walipata bao lao la kwanza kupitia kwa Alfred Mfongang na dakika tano baadaye mchezaji mwenzake Isama Mpeko akatolewa nje baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.

Azam walitumia vyema upungufu huo kwa kusawazisha kupitia kwa John Bocco dakika ya 68 na Mrisho Ngassa akapachika bao la ushindi dakika ya mwisho wa mchezo.

Nao Yanga walipata bao lao dakika ya 13 ya kipindi cha nyongeza kupitia kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda Hamis Kiiza.

Kiiza alifunga bao zuri la kichwa kufuatia mpira kutoka kwa Haruna Niyonzima, ambaye ni mchezaji wa kulipwa kutoka Rwanda.

Yanga na Azam watacheza fainali Jumamosi, mechi ambayo itatanguliwa na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya Vita na APR.