Wachezaji watimuliwa mashindanoni

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Michel Morganella

Timu ya mpira wa miguu ya Uswizi imemfukuza beki wake Michel Morganella kutoka mashindanoni kwa kutuma ujumbe wa ki-ubaguzi wa rangi akitumia mtandao wa Twitter.

Mchezaji huyo alituma ujumbe ukiwalenga watu wa Korea ya kusini kwa ujumla kupitia Twitter baada ya Timu yake kupoteza mechi dhidi ya Korea ya kusini 2-1 jumapili iliyopita.

Tangu hapo mtandao huo umefutwa na beki huyo kuomba radhi, akisema kweli, nilikosea sana baada ya matokeo yasiyoridhisha, alisema kijana huyo mwenye umri wa miaka 23.

Morganella aliongezea kusema kua: "ningependa kuwaomba radhi raia wote wa Korea ya kusini na timu yao, vilevile ujumbe wa Uswizi na mchezo wa mpira kwa ujumla nchini Uswizi."

Mapema mwezi huu, mwanariadha wa Ugiriki wa kuruka hatua tatu kuelekea mchangani Paraskevi Papachristou alitimuliwa kutoka kwenye kikosi cha Olimpiki cha nchi yake kufuatia matamshi aliyoyatoa kupitia Twitter yaliyoonekana kuwa ya kiubaguzi wa rangi.

Kocha mkuu wa Kikosi cha Uswizi Gian Gilli alisema kua Morganella, anayecheza soka yake ya kulipwa na klabu ya Italia -Palermo ameidhalilisha timu nzima. Kocha huyo amesema kua alibagua, katukana na kukiuka hadhi ya raia na wachezaji wa timu nzima ya Korea ya kusini.