Bolt aingia nusu fainali mita 200

Usain Bolt ameanza vyema juhudi zake za kuchukua tena medali nyingine ya dhahabu katika mbio fupi za mita 200, huku akiwa tayari akiwa na ile ya dhahabu katika mbio za mita 100.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Anatazamiwa kuweka kibindoni medali ya mita 200

Bolt alifuzu kuingia mbio za nusu fainali, mita 200, kwa muda wa sekunde 20.39.

Wanariadha wenzake kutoka nyumbani Jamaica, Yohan Blake na Warren Weir pia walifuzu.

Wengine waliofanikiwa kuingia nusu fainali ni Mmarekani Wallace Spearmon, Mfaransa Christophe Lemaitre na Muingereza Christian Malcolm.

Muingereza James Ellington alishindwa kufuzu kuingia nusu fainali, baada ya kumaliza katika nafasi ya sita.

Mbio za nusu fainali mita 200 ni Jumatano, na fainali ni Alhamisi.

Bolt, bingwa mara nne katika mashindano ya Olimpiki, na aliyefanikiwa kuutetea ubingwa wake wa mjini Beijing kikamilifu Jumapili katika mbio za mita 100, atajaribu tena kuhifadhi ubingwa katika mbio za mita 200 pia.

Akizungumza na waandishi wa michezo wa BBC, Bolt alisema: "Kuna mashabiki wa ajabu, na wana jukumu muhimu sana katika mbio ninazoshiriki, na mimi huzipenda sana mbio za mita 200".

"Mimi hujaribu kutimiza wajibu wangu, ninaelewa kila kinachofuatia ushindi, kwa hiyo ni lazima nifurahie kile ninachokifanya".

Blake, ambaye alipata medali ya fedha kwa kumaliza wa pili nyuma ya Bolt katika mbio za mita 100, pia alifuzu vyema kuingia nusu fainali ya mbio za mita 200, akiandikisha muda wa sekunde 20.38.

Blake alielezea: "Ninajihisi nimo katika hali nzuri mno. Yote ni kutokana na kocha, na mbio za mita 100 zimenifundisha mengi."

"Ilikuwa ni medali yangu ya kwanza katika mbio za Olimpiki. Mimi hufurahia zaidi mbio za mita 200, na ninaweza kuvumilia zaidi muda huo mrefu."