Meneja wa Blackburn kutimuliwa?

Mshauri wa club ya Blackburn Shebby Singh amesema meneja Steve Kean wa club hiyo, atatimuliwa iwapo timu hiyo itapoteza mechi zake tatu za kwanza katika msimu.

Alipoulizwa katika mkutano na mashabiki wa timu hiyo kama Kean ataondolewa iwapo watapoteza michezo mitatu ya kwanza, Singh alijijibu: "Ndiyo."

Lakini Singh aliongeza kuwa hatakurupuka kutoa uamuzi juu ya Kean.

"Itategemea na matokeo," amesema Singh, mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Malaysia aliyeletwa katika klabu hiyo ya Ewood Park na wamiliki wake Venky mwezi June.

''Iwapo baada ya mechi tatu, tumepoteza pointi tisa, tutakuwa na asilimia hamsini tu ya kusonga mbele.

Kean amekuwa akikosolewa na baadhi ya mashabiki wa Blackburn ambao wamekuwa wakifanya maandamano ya mara kwa mara kumpinga Kean na wamiliki wa klabu hiyo.

Rovers walidhalilishwa katika Premier League mwishoni mwa msimu uliopita lakini Kean aliendelea kushika nafasi yake.

Toka wakati huo amewasajili wachezaji saba akiwemo Leon Best kwa kitita cha pauni milioni tatu, Danny Murphy kwa uhamisho usio na malipo na Dickson Etuhu kwa kitita ambacho hakikutangazwa wazi.