Mo Farah apata dhahabu tena

Mo Farah alijiongezea medali nyingine ya dhahabu siku ya Jumamosi kwa kuibuka bingwa katika fainali ya mbio za mita 5000.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Sasa amepata medali za dhahabu za Olimpiki katika mbio za mita 5,000 na 10,000

Farah, mwenye umri wa miaka 29, awali katika mashindano ya Olimpiki ya London alikuwa tayari amechukua medali katika mbio za mita 10,000.

Ushindi huo uliiwezesha Uingereza kupata medali 27 za dhahabu siku ya Jumamosi, na jumla ya medali 60.

Farah aliongeza juhudi zaidi katika mzunguko wa mwisho, kufuatia upinzani mkali, na kukamilisha mbio kwa muda wa dakika 13, sekunde 41.66.

Mwanariadha wa Ethiopia Dejen Gebremeskel aliondoka na medali ya fedha, huku Mkenya Thomas Longosiwa akipata ya fedha.

Wiki moja iliyopita ushindi wa Farah katika mbio za mita 10,000 uliwaacha mashabiki wengi wa riadha wakizungumzia kuhusu fainali za kusisimua siku ya Jumamosi katika mbio za mita 5,000.

Kabla ya fainali hiyo ya 5,000, Farah alikuwa katika nafasi ya 11 ulimwenguni, katika orodha ya wanariadha bora duniani, kwa kuzingatia mashindano mbalimbali msimu huu.

Wanariadha saba katika orodha hii walikuwa wamejiandikishia muda bora zaidi wa kibinafsi katika mashindano walioshiriki.

Lakini kufuatia Farah kupata medali ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 katika mashindano ya dunia ya riadha ya Daegu, alifahamu fika kwamba ana uwezo wa kutwaa dhahabu pia katika michezo ya Olimpiki ya London.

Vile vile alielewa kwamba itabidi aufanyie mwili wake kazi ya ziada, ili aweze kupumzika ya kutosha, kabla ya kuwania ubingwa wa mbio za mita 5,000, baada ya uchovu kufuatia ushindi wa mbio za mita 10,000, na kwa mara nyingine kupambana tena na baadhi ya wanariadha bora zaidi duniani.