Gernot Rohr achaguliwa kocha wa Niger

Imebadilishwa: 5 Septemba, 2012 - Saa 14:04 GMT
Kocha mpya wa Niger

Kocha mpya wa Niger

Gernot Rohr ndiye meneja mpya wa timu ya taifa ya soka ya nchi ya Niger.

Rohr, raia wa Ujerumani, ataiongoza timu hiyo kwa mara ya kwanza katika mechi ya Jumapili ugenini dhidi ya Guinea, hii ikiwa ni mechi yao ya mwisho ya kufuzu kushirikishwa katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2013.

Rohr amechukua kibarua ambacho awali kilishikiliwa na raia wa Ufaransa, Roland Courbis.

Kocha mpya Rohr alitoa mafunzo kwa timu ya Gabon, wakati iliposhirikiana na nchi jirani ya Guinea, kama wenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mapema mwaka huu.

Lakini Gabon ilipoondolewa katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo, Rohr hakupata mkataba mpya.

Rohr, mwenye umri wa miaka 59, alipokuwa mchezaji, aliweza kuichezea Bayern Munich ya Ujerumani, na Girondins Bordeaux ya Ufaransa, na alikuwa akiifunza Bordeaux, mwaka 1996 katika mashindano ya Kombe la UEFA, iliposhindwa katika fainali na Bayern.

Aliwahi pia kuwa meneja wa vilabu vya Ufaransa, Nantes na Nice, akasonga hadi Young Boys Berne ya Uswisi, na vile vile klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.

Chama cha soka cha Niger hakikutoa maelezo zaidi kuhusiana na mkataba huo.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.