Weir ajiiandika shujaa wa London 2012

Imebadilishwa: 9 Septemba, 2012 - Saa 15:11 GMT

David Weir

Wakati tukitazamia sherehe ya kuhitimisha mashindano ya Paralympics, riadha kwa walemavu hii leo. Mbio zilizochangamsha watazamaji waliosimama kanda mwa barabara za Jiji la London mapema leo wamejionea kujitolea kwa washiriki waliopamba mji huu kushiriki mbio za marathon kuanzia sehemu ijulikanayo kama The Mall hatua chache kutoka kasri ya Malkia ya Buckingham.

Na timu ya Uingereza maarufu kama Team GB iliyoazimia kumaliza mashindano haya ya Paralympics kwa kuzoa medali za kutosha kumaliza katika nafasi ya pili imehitimisha tamaa yao kwa ushindi wa medali ya dhahabu ya mwisho iliyonyakuliwa na shujaa wa Uingereza na mashindano haya David Weir aliyemaliza na kukamilisha ushindi wa mashindano matatu.

Weir alishiriki marathon baada ya kushinda mara tatu kwenye mashindano ya mwaka huu mjini London na hivyo kuongezea medali ya nne ya dhahabu.Weir mwenye umri wa miaka 33 alishiriki na kushinda mbio za mita 800, 1500 na 5000 na leo aliongezea medali ya 4 ya dhahabu.

Hali ya hewa yenyewe haikuwa nzuri kwa mtu yeyote kukiwa na joto kali la majira haya ya joto. Weir mwenyewe alionekana kama aliyechanganyikiwa mwishoni mwa mashindano bila kutambua msitari unaobainisha mwisho wa mbio ingawa rangi nyeupe iliyoandikwa ilikua wazi lakini mwishowe alipopanda jukwaa kupokea medali yake hakusahau tabasamu na shangwe zilizofuata na kuashiria shujaa wa Uingereza wa mashindano haya ya Paralympics mwaka 2012 mjini London.

Oscar Pistorius

Kwa upande wa wanawake team GB iliwakilishwa na Shelly Woods katika mbio za T54 Marathon. Ingawa Shelly Woods alionekana kama aliyechukizwa mashindano ya awali baada ya kushindwa katika juhudi zake, imani yake ilikua katika mbio za marathon hii leo na dhamira yake ikawa kushinda medali.

Na hivyo ndivyo alivyojipanga na kuendesha baiskeli lake bila kutetereka akipitia mitaa ya mji wa London iliyojaa mashabiki waliomtakia ufanisi na hilo labda lilichangia kwake kustahamili maili 26 na joto la kupindukia akimaliza wa pili na hivyo kuridhika na medali ya fedha.

Katika mbio za mwisho kutoka uwanja wa Olimpiki zilikua za mita 400 wanaume na mkimbiaji kutoka Afrika ya kusini anayetumia miguu mbadia ya chuma Oscar Pistorius aliandika jina lake miongoni mwa miamba ya mashindano ya riadha kwa kuondoka na dhahabu.

Hiyo ikawa medali yake ya pili kwenye mashindano haya baada ya ile aliyoshinda kupitia mbio za mita 100 kupokeza vijiti na katika wiki ambamo alishindwa kutetea taji lake la mita 100 na 200.

Pistorius ndiye mlemavu maarufu kuliko wote kutokana na sifa yake ya kushiriki mashindano ya Olimpiki kwa watu wasio na ulemavu na vilevile walemavu ya Paralympic.

Kwenye mashindano haya ya London mkimbiaji huyo amepitwa na umahiri wa Weir aliyeshiriki na kushinda mashindano yake akitumia baiskeli ya walemavu ambaye jumapili hii amevuna medali ya nne.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.