Cameron aomba radhi

Imebadilishwa: 12 Septemba, 2012 - Saa 23:12 GMT
Liverpool

Uchunguzi wa awali uliwalaumu mashabiki wa Liverpool uliosababisha vifo vya mashabiki 96

David Cameron ameomba radhi na kuelezea kama hali ya “kutotendewa haki maradufu” kufuatia maafa ya Hillsborough katika uwanja wa soka.

Akizungumza baada ya kusoma ripoti huru ambayo ilifichua baadhi ya maelezo ambayo hayakuwa yamewekwa wazi hapo awali kufuatia mkasa huo, waziri mkuu wa Uingereza alisema maafisa wa polisi walishindwa kutekeleza wajibu wao kikamilifu, na kisha kuwalaumu mashabiki wa klabu ya Liverpool.

Mashabiki 96 walikufa kufuatia taharuki uwanjani na kukanyagana, katika uwanja wa Sheffield Wednesday, mwaka 1989.
Trevor Hicks, ambaye ni kati ya watu ambao wamekuwa wakiongoza kampeni ya kufahamu ukweli, alisema ripoti hiyo inaonyesha kwamba maisha ya wengi yangeliweza kuokolewa kama huduma za dharura zingelipatikana kwa haraka mara tu baada ya mashabiki kuanza kukanyagana.

Bwana Hicks, ambaye binti zake wawili walifariki katika mkasa huo, alisema sasa wao watashinikiza hatua za kisheria kufuatia makosa ya kihalifu zichukuliwe katika kuhakikisha waliohusika wataadhibiwa.

"Tunahisi tumepiga hatua mbele. Ukweli umepatikana leo, na haki inaanza kesho," alielezea.
Ripoti hiyo imetayarishwa na tume huru ya Hillsborough iliyokabidhiwa jukumu la kuchunguza chanzo cha maafa hayo, na ambayo ilipitia zaidi ya kurasa 450,000 za maelezo mbalimbali, katika kipindi cha miezi 18.

Familia za waliokufa kwa muda mrefu zilipinga maelezo ya awali kwamba wote ya waliofariki walikuwa tayari wamekata roho dakika 15 baada ya mechi kuanza saa tisa, au ubongo ulikuwa tayari umeshakufa.

Anne Williams anadai kwamba mwanawe Kevin bado alikuwa hai saa kumi siku ya mkasa, na ameitaka serikali kuanzisha uchunguzi mpya kuhusiana na kifo chake.

Jopo hilo ambalo liliendesha uchunguzi lilielezea kwamba kati ya watu 28 ya wale 96 waliokufa, sio kweli kwamba walikuwa na damu iliyoganda na kutoweza kuenea mwilini, na kuna ushahidi ambao unaonyesha kwamba watu 31 walikuwa na mioyo na mapafu ambayo bado yalikuwa yanafanya kazi hata baada ya mkanyagano.

Mshauri wa masuala ya matibabu katika jopo hilo, Dk Bill Kirkup, alieleza kwamba watu 41 kati ya 96 waliokufa wangeliweza kuokolewa kama wangelipata matibabu kwa haraka.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.