Arsenal kupambana na Olympiakos

Imebadilishwa: 3 Oktoba, 2012 - Saa 13:32 GMT
Arsenal

Vijana wa Arsenal watachezea uwanja wa nyumbani wa Imarati dhidi ya Olympiakos

Jioni ya Jumatano kuna mechi nane za klabu bingwa barani Ulaya, na kati ya hizo ni Arsenal kuialiki timu ya Ugiriki ya Olympiakos katika uwanja wa Imarati.

Arsenal hata hivyo huenda ikazikosa huduma za Mikel Arteta, wakati wageni wao watakapofika katika mechi hiyo ya kundi A.

Mchezaji huyo kutoka Uhispania, mwenye umri wa miaka 30, anauguza jeraha katika kifundo cha mguu, na atakaguliwa tena kabla ya mechi kufahamika kama atacheza au la.

Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger, pia ameelezea kwamba kipa Wojciech Szczesny "atahitaji wiki mbili hadi wiki tatu hivi" ili naye aweze kupata nafuu kutokana na jeraha la kifundo cha mguu.

Kiungo cha kati Abou Diaby naye hataweza kucheza kwa kipindi cha wiki tatu, kutokana na misuli ya paja iliyomsumbua tangu alipoondoka uwanjani katika pambano la Jumamosi dhidi ya Chelsea katika mechi ya ligi kuu ya Premier.

Kiungo cha kati mwenzake, Tomas Rosicky, pia hayumo katika hali nzuri, baada ya kuumia katika mechi ya Euro 2012.

Bacary Sagna, ambaye anacheza katika eneo la ulinzi upande wa kulia uwanjani, amerudi mazoezini kikamilifu, lakini hajawahi kucheza tangu Mei 5, alipovunjika mguu katika mechi dhidi ya Norwich.

Jack Wilshere, alicheza mechi yake ya kwanza baada ya miezi 14 siku ya Jumatatu, kwa muda wa dakika 63, dhidi ya timu ya West Brom, katika mechi ya ligi kuu ya Premier kwa vijana chini ya umri wa miaka 21.

"Aliondoka uwanjani pasipo tatizo," alieleza Wenger, kufuatia mchezaji huyo wa miaka 20 kurudi uwanjani baada ya muda mrefu.

Kwa hiyo, licha ya Arsenal kuhofia itawakosa baadhi ya wachezaji wazoefu, matumaini ya Arsenal kupata ushindi sio haba.

Mechi nyingine za Jumatano usiku ni pamoja na timu nyingine ya Uingereza, Manchester City, kucheza dhidi ya Borussia Dortmund ya Ujerumani.

Dynamo Kiev ya Ukraine kucheza dhidi ya Dinamo Zagreb ya Croatia.

FC Porto ya Ureno itapambana na Paris Saint Germain ya Ufaransa.

Schalke ya Ujerumani wanakutana na klabu nyingine ya Ufaransa, Montpellier.

Zenit St Petersburg ya Urusi nayo itacheza na AC Milan ya Italia, huku Anderlecht ya Ubelgiji ikicheza na Malaga ya Uhispania.

Katika pambano lingine, Ajax ya Uholanzi itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Real Madrid ya Uhispania.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.