Wanamichezo wa jinsia moja

Imebadilishwa: 11 Oktoba, 2012 - Saa 16:21 GMT
Greg Louganis

Louganis alipoumizwa na ubao akiogelea mwaka 1988 mjini Seoul

Nepal itakuwa ni nchi ya kwanza Asia ya Kusini kuwa mwenyeji wa mashindano ya wanamichezo wanaoshiriki katika mapenzi ya jinsia moja, wale wanaovutiwa na wanawake na vile vile wanaume, na pia wale ambao wamebadilisha jinsia moja hadi nyingine.

Mashindano hayo, yanayojulikana kama lesbians, gays, bisexuals, transgendered and intersexes, kwa kifupi LGBTI, ni mashindano ya siku tatu ambayo yanaanza Ijumaa.

Zaidi ya wanamichezo 350 watakuwa ni kutoka Nepal, na wengine 150 watakuwa ni kutoka mataifa 17 kote ulimwenguni.

Kati ya wanariadha wanaofahamika ni pamoja na mwanamichezo maarufu wa Olimpiki, Gregory Efthimios Louganis, ambaye anajulikana zaidi miongoni mwa mashabiki wa michezo kama Greg Louganis.

Mwogeleaji huyo wa Marekani, ambaye alishinda medali mbili mbili katika mashindano ya Olimpiki miaka ya 1984 na 1988, amekubali atafika katika mashindano hayo ya Kathmandu kama mgeni mheshimiwa.

Louganis anafahamika kwa kuwasaidia wanamichezo kuimarisha vipawa vyao kote ulimwenguni, na kuwepo kwake katika mashindano hayo ni jambo ambalo linasemekana litayapa uzito.

Mashindano hayo pia yatawapa nafasi ya wanaoshiriki katika mashindano ya LGBTI kuendelea kuzitetea haki zao, hasa nchini Nepal, walielezea waandalizi kutoka shirika la Blue Diamond Society.

Kati ya yale yanayokumbukwa kumhusu mwanariadha Louganis ni wakati alipoumizwa na ubao alipokuwa anaruka majini katika mashindano ya Olimpiki mjini Seoul, mwaka 1988.

Licha ya kuumia na kushonwa kichwa, alifanikiwa kushiriki katika mashindano, na akawa mshindi.

Baadaye iligunduliwa kwamba miezi sita kabla ya mashindano ya Olimpiki, kumbe alikuwa akiishi kwa viini vya HIV.

Louganis alifichua mwaka 1994 kwamba alikuwa akishiriki katika mapenzi ya jinsia moja, na aliandika kitabu, 'Breaking the Surface', akielezea baadhi ya masaibu yaliyompata mapema maishani, ikiwa ni pamoja na kukandamizwa, kutomaswa na akiishi katika hali ya kusononeka mno maishani.


BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.