Sifa za Christopher Katongo

Imebadilishwa: 22 Novemba, 2012 - Saa 10:12 GMT
Christopher Katongo

Christopher Katongo

Miaka 10 imekuwa ya mafanikio makubwa kwa nahodha wa timu ya taifa ya Zambia, Christopher Katongo.

Zambia ni mabingwa wa kombe la mataifa ya Afrika wa mwaka 2012.

Chris Katongon alianza kunga'ara katika timu yake ya Green Buffaloes ya Zambia kati ya mwaka 2003 na 2004.

Moja ya ushindi mkubwa alioupata katika uchezaji wake katika timu ya Buffaloes ni karamu ya magoli manne aliyofunga katika mechi moja mwaka 2003 na kufuatiwa na ushindi wa magoli 5-0 na 6-1 katika kombe la Shirikisho dhidi ya timu za Saint Michel ya Ushelisheli na Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Hata hivyo, tofauti na wachezaji wenzake wa timu ya Zambia, ambao walianza kuvuma katika michezo ya wachezaji wa chini ya umri wa miaka 17 na 20, umaarufu wa Katongo kuingia katika timu ya taifa maarufu kama Chipolopolo ulichelewa.

Kwanza aliingia timu hiyo akiwa katika kikosi cha wachezaji chini ya umri wa miaka 23.

Katongo alikuwa miongoni mwa wachezaji wa timu ya Zambia, katika michezo ya Afrika ya mwaka 2003, wakati timu hiyo iliposhika nafasi ya nne katika michezo hiyo iliyoandaliwa mjini, Nigeria, akifunga goli moja katika michezo hiyo na lingine katika hatua ya kufuzu.

Alicheza mechi yake ya kwanza katika mashindano ya kombe la mataifa bingwa barani Afrika nchini Misri, mwaka 2006 ambako Zambia ilitolewa katika hatua ya makundi huku akifunga goli moja kwa sifuri dhidi ya Afrika Kusini.

Mwaka mmoja baadaye, alifunga magoli matatu katika mechi moja dhidi ya Afrika Kusini, Zambia ilipopata ushindi wa magoli 3-1 katika mechi iliyochezwa mjini Cape Town na kuiwezesha Zambia kufuzu kwa fainali ya kombe la mataifa Bingwa barani Afrika mwaka 2008.

Wakati huo huo, uchezaji wake ulimfikisha katika timu ya Jomo Cosmos ya Afrika Kusini, ambako alicheza kutoka mwaka 2004 hadi 2007.

Kisha alijiunga na klabu ya Brondby nchini Denmark mwaka 2007 na baadaye alihamia Ujerumani katika klabu ya Arminia Bielefeld mwaka 2008.

Mwaka 2010, aliondoka Ujerumani na kwenda Ugiriki ambako alicheza kwa mwaka mmoja na klabu ya Skoda Xanthi na baadaye kwenda Uchina mwaka 2011 na kujiunga na timu yake ya sasa ya Henan Construction.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.