Ferguson achukizwa na ulinzi

Imebadilishwa: 1 Disemba, 2012 - Saa 23:37 GMT
Reading na Man United

Reading ikiwa nyumbani iliwasumbua mno Manchester United

Sir Alex Ferguson, meneja wa Manchester United, Jumamosi alielezea kwamba hajawahi kuona ulinzi mbovu wa timu yake msimu huu kama alivoshuhudia wakati timu yake ikiwa ugenini Reading, licha ya kuondoka na ushindi wa magoli 4-3 dhidi ya wenyeji.

United mara nyingi walionekana dhaifu kutokana na mchezo wa kupanga na kuviziana, na meneja Ferguson alisema ni lazima timu yake kuinua kiwango cha mchezo wao kufikia mwishoni mwa wiki ijayo, wakati watakutana na majirani Manchester City.

"Ulikuwa ni ulinzi mbovu zaidi msimu huu," alielezea Ferguson.

“Lazima tuchukue hatua kuhusu hili”.

"Reading waliweza kuelekeza mipira vyema, lakini kabisa mlikuwa hamna ushindani katika kuzuia hayo."

Mara mbili walilemewa na kuwaacha Reading kutangulia kwa magoli, na hii ikiwa ni mara ya 14 msimu huu kuiacha timu ya upinzani kutangulia kupata bao la kwanza.

Magoli yote saba ya timu zote mbili yalifungwa katika dakika 34 za kipindi cha kwanza katika uwanja huo wa Madejski.

Kwa bahati nzuri, Man U waliweza kujibu mashambulizi ya Reading mara mbili, na kuongezea magoli ambayo yaliwawezesha kurudi Old Trafford na ushindi, na wakiwa kileleni mwa ligi ya Premier, sasa tofauti kati yao na wapinzani wao wakuu, majirani Man City, ni pointi tatu.

Man City, wakiwa nyumbani katika uwanja wao wa Etihad, watawakaribisha Man United Jumapili ijayo.
"Tulistahili kutandikwa leo," alisema Ferguson.

"Hakuna aliyefanya juhudi za kushindania migongeo. Pasipo kupendelea, Reading walimiliki mpira vyema, kijana [Nicky] Shorey aliwaelekezea wenzake mipira vyema mno. Tulistahili kufanya vyema zaidi ya hivyo. Tulicheza vibaya mno”, alilalama Ferguson.

"Iwapo utafanya makosa kama hayo katika ulinzi, basi kila wiki kazi yako itakuwa ni juhudi za kuokoa tu. Leo ilikuwa ni juhudi zaidi za kuokoa tu.
"Ilikuwa ni muujiza namna tulivyoshinda kwa ulinzi kama huo. Ninaridhika tu kwa kuwa tuliondoka na ushindi.”

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.